• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:55 PM
Klabu za Barcelona, Juventus na Real Madrid zaendelea kupigania mpango wa kuanzishwa kwa European Super League

Klabu za Barcelona, Juventus na Real Madrid zaendelea kupigania mpango wa kuanzishwa kwa European Super League

Na MASHIRIKA

BARCELONA, Real Madrid na Juventus wameshikilia kwamba wataendelea na mpango wao wa kushinikiza kuwepo kwa kipute kipya cha European Super League (ESL) huku wakidai kuwa wamejitetea vilivyo dhidi ya adhabu yoyote kutoka Shirikisho la Soka la Bara Ulaya (Uefa).

Katika taarifa ya pamoja mnamo Julai 30, 2021 katika jiji la Madrid nchini Uhispania, vikosi hivyo vitatu vilisisitiza kuwa Uefa wana ulazima wa kusitisha taratibu zote za kinidhamu dhidi yao.

Uefa ililegeza msimamo dhidi ya klabu hizo mnamo Juni baada ya kesi dhidi ya Barcelona, Juventus na Real Madrid kuhamishwa hadi Mahakama ya Malalamishi ya Spoti barani Ulaya.

Jumla ya vikosi 12 vilikuwa vimehusishwa katika mchakato wa kubuniwa kwa ESL mnamo Aprili ila mpango huo ukasambaratishwa saa 72 baadaye vikosi tisa vilipojiondoa kutokana na malalamishi ya mashabiki, klabu nyinginezo za ligi mbalimbali na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Juventus, Barcelona na Real Madrid ndizo klabu za pekee ambazo hazikujiondoa kwenye mpango huo na badala yake, zimekuwa zikisisitiza kuwa kuna mikakati ya kuimarishwa zaidi kwa juhudi za kuundwa kwa kivumbi kipya cha ESL.

Klabu tisa zilizojiondoa kwenye ESL ni Manchester City, Chelsea, Manchester United, Liverpool, Arsenal, Tottenham, Inter Milan, AC Milan na Atletico Madrid. Ziliadhibiwa kifedha na Uefa mnamo Mei 2021.

Kila mojawapo ya klabu hizo tisa zilizoadhibiwa na Uefa zinastahili sasa kutoa kima cha Sh1.8 bilioni ambazo zitasambazwa kwa watoto kutoka familia zisizojiweza na akademia za wanasoka chipukizi kutoka timu za mashinani barani Ulaya.

Aidha, kila klabu itashuhudia asilimia tano ya mapato kutokana na ushiriki wa mechi za bara Ulaya ikiondolewa na Uefa kuanzia msimu wa 2023-24. Fedha hizo zitatengewa maendeleo ya soka ya mashinani katika mataifa mbalimbali ya bara Ulaya.

Mbali na kutozwa Sh1.8 na asilimia tano ya mapatano ya kushiriki vipute vya UEFA na Europa League kuondolewa kuanzia 2023-24, kila mojawapo ya klabu tisa kati ya 12 zilizohusishwa kwenye uasisi wa ESL zimepigwa faini ya Sh12 bilioni.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

Agala na Makokha wamaliza voliboli ya ufukweni Olimpiki...

BADO SWARA! Kenya yaona vimulimuli dhahabu ya mbio za...