• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
KAMAU: Ufanisi wa nchi unategemea viongozi tunaowachagua

KAMAU: Ufanisi wa nchi unategemea viongozi tunaowachagua

Na WANDERI KAMAU

KULINGANA na mafundisho ya vitabu vitakatifu, Yesu Kristo na Mtume Mohammed walikataliwa na baadhi ya wafuasi licha ya sifa za wema wao.

Kwa wakati mmoja, Mtawala Pilato aliwauliza wenyeji wa mji wa Yerusalemu kuhusu mtu ambaye wangetaka aachiliwe kutoka gerezani kati ya Yesu na mwizi aliyeitwa Baranaba.

Kwa umoja wa aina yake, watu hao waliungana kumshinikiza mfalme kumwachilia Barnabas, wakishikilia kuwa “yeye ni mmoja wao.”

Walimwambia mfalme kumsulubisha Yesu, kwani “hawakumfahamu na hakuwa mmoja wao.”

Taswira hiyo inafanana na siasa za Kenya na nchi nyingi zenye chumi za kadri duniani.

Wananchi huwa wanawakataa viongozi wenye sifa nzuri za utendakazi na kuwachagua wanasiasa wasiowajali hata kidogo.

Mtindo huu ndio umekuwa ukizifanya nchi nyingi kubaki nyuma kimaendeleo katika nyanja zote.

Mfano halisi ni Kenya, ambapo katika miaka ya sitini, tulikuwa katika kiwango sawa cha ukuaji wa kiuchumi na nchi kama Malaysia na Singapore.

Kulingana na wasomi wa historia, Kenya ilikuwa miongoni mwa mataifa yaliyopigiwa upatu kupata ukuaji mkubwa wa kiuchumi sana barani Afrika baada ya wakoloni kuondoka.

Hili ni kutokana na msingi mzuri wa kisiasa na kiuchumi ambao uliwekwa na Mzee Jomo Kenyatta katika miaka ya mwanzo mwanzo ya utawala wake.

Hata hivyo, hali ilianza kubadilika, kadri miaka ilivyosonga. Ufisadi ulianza kukithiri serikalini. Viongozi waliojitokeza kuwakashifu wanasiasa waliotajwa kwenye sakata za ufisadi walitishiwa maisha yao. Taharuki ilitanda nchini. Wananchi nao wakajawa na hofu.

Mauaji yalifuata “kuwanyamazisha” viongozi walioendelea kuikashifu serikali kutokana na ufisadi.

Vifo. Vifo na mikasa isiyoeleweka. Waliuawa Pio Gama Pinto, Tom Mboya, JM Kariuki kati ya wazalendo wengine waliosimama kidete kuukabili utawala wa Mzee Jomo Kenyatta.

Wakati mauaji hayo yalikithiri nchini, taifa kama Singapore lilikuwa likiendesha mikakati thabiti sana kupiga jeki uchumi wake.

Taifa hilo ndogo lilipiga hatua hizo kubwa kupitia uongozi wa Lee Quan Yew, aliyeanzisha sera kali za kufufua viwanda na kuwashirikisha wananchi kwenye shughuli za kuikuza nchi.

Kwa sasa, Kenya na Singapore ni kama mbingu na nchi—haziwezi kuonana hata kidogo.

Wakati Singapore inaorodheshwa kuwa miongoni mwa nchi zenye chumi thabiti zaidi duniani, Kenya bado inaandamwa na mzigo wa mikopo ya kimataifa.

Ujumbe kwa Wakenya: Jibu la ufanisi wa nchi limo kwenye aina ya uongozi unaochaguliwa.

[email protected]

You can share this post!

MUTUA: Chocheo la vita Ethiopia ni ukabila, manyanyaso

BURUDANI: Daisy apania kutinga upeo wa Gal-Gadot Varsano