• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:36 PM
JAMVI: Hofu waliohamia Tangatanga ni ‘majasusi’

JAMVI: Hofu waliohamia Tangatanga ni ‘majasusi’

Na WANDERI KAMAU

LICHA ya baadhi ya wanasiasa kutangaza kuhamia katika mrengo wa ‘Tangatanga’ kutoka ‘Kieleweke’ na mirengo mingine ya kisiasa nchini, imeibuka kuwa baadhi yao wanaonekana kama “majasusi” wa kisiasa.

Ni hali ambayo imezua wasiwasi katika kundi hilo ambalo huwa linamuunga mkono Naibu Rais William Ruto, baadhi ya washirika wakuu wakisema wanapaswa kutahadhari kuhusu wanasiasa wanaotangaza kujiunga nao ama kurejea kwenye mrengo huo.

Katika siku za hivi karibuni, baadhi ya wanasiasa ambao wametangaza hadharani kurejea katika kundi hilo ni wabunge David Gikaria (Nakuru Mashariki) na Catherine Waruguru (Laikipia).

Wawili hao walikuwa wanachama wa kundi hilo kabla ya kugura na kujiunga na ‘Kieleweke.’

Wale ambao wametangaza kugura ‘Kieleweke’ na kujiunga na ‘Tangatanga’ katika siku za hivi karibuni ni wabunge Gathoni wa Muchomba (Kiambu), Kago wa Lydia (Githunguri) na Samuel Gacobe (Subukia).

Naibu Rais William Ruto akijibu salamu za wananchi alipowasili katika Shule ya Msingi ya Mary Immaculate iliyoko Laikipia akiwa na Catherine Waruguru (kulia) na Spika wa Seneti Ken Lusaka miongoni mwa viongozi wengine Juni 9, 2018. Picha/ Joseph Kanyi

Hata hivyo, hatua ya kurejea kwa wabunge Waruguru na Gikaria ndiyo imezua hofu katika mrengo huo, baadhi ya wabunge wakieleza tashwishi yao kuwa huenda wakawa “mawakala wa wapinzani wao.”

Kwenye mahojiano na Jamvi la Siasa, mshirika mmoja wa ‘Tangatanga’, alisema ni kinaya kuwa wabunge hao wanarejea katika kambi hiyo baada ya kutumia muda wao kumkosoa vikali Dkt Ruto na mipango yao kwa jumla.

“Hawa si watu wa kuaminika hata kidogo. Walikuwa nasi mwanzoni japo wakavuka katika mrengo pinzani. Wamekuwa wakitazama tukihangaishwa na serikali bila yao kututetea kwa namna yoyote ile. Wengine hata waligeuka na kuanza kumtusi Dkt Ruto. Ni vipi tena tunaweza kuwaamini?” akashangaa mbunge huyo ambaye hakutaka kutajwa.

Wasiwasi mkuu ulio katika ‘Tangatanga’ kuwa huenda wabunge wanaojiunga nao kwa kisingizio cha “kugura” ‘Kieleweke’ wakafichua mipango na mikakati ya kisiasa na Dkt Ruto, siri ambazo serikali itazitumia baadaye kuwahangaisha.

Baada ya kuhama kutoka ‘Tangatanga’ na kujiunga na Kieleweke, Bi Waruguru alimtaja Dkt Ruto kama “mwanasiasa mwongo na mnafiki, ambaye hapaswi kuaminiwa na yeyote.”

Bi Waruguru alitangaza kujitoa ‘Tangatanga’ Agosti mwaka uliopita, siku chache baada ya kukutana na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, aliyemtaja kuwa “mwanga wa kisiasa utakaowaongoza Wakenya kuelekea Kanani.”

“Niliondoka katika Tangatanga baada ya kugundua kuwa Dkt Ruto anapigania maslahi yake binafsi wala si ya ukanda wa Mlima Kenya. Niligundua pia kuwa wanasiasa wengi ambao wanamfuata ni kama wanashurutishwa kufanya hivyo, wala si maamuzi yao huru,” akasema Bi Waruguru.

Tangu wakati huo, mbunge huyo amekuwa akimsifu Rais Kenyatta, akimtaja kuwa mwanasiasa shupavu, atakayeleta mabadiliko kamili ya kisiasa na kiuchumi kabla ya kustaafu kwake.

Kama “zawadi” ya kumwasi Dkt Ruto, Bi Waruguru aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo.

Kutokana na mwelekeo huo, mbunge Rigathi Gachagu (Mathira) anasema ikiwa kutaibuka nafasi katika mrengo wa Tangatanga, basi wale “waliovumilia kuhangaishwa na serikali ndio wanaopaswa kuzingatiwa kwanza.”

“Taswira iliyopo ni kama zoezi la kujenga nyumba. Kuna baadhi ya wajenzi waliotutoroka tulipokuwa tukiweka msingi wa nyumba yetu, ijapokuwa sasa wanataka kurejea wakati tuko karibu kuikamilisha. Hatutawafukuza wakirejea. Hata hivyo, lazima nafasi zitakazoibuka zikabidhiwe wale ambao wamevumilia mateso ambayo tumekuwa tukielekezwa na serikali,” akasema mbunge huyo.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga akiwa na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Laikipia Catherine Waruguru (kushoto) Juni 09, 2020 katika Capitol Hill, Nairobi. Picha/ Maktaba

Licha ya hayo, wadadisi wa siasa wanasema kuwa sababu kuu ya mwelekeo huo ni ubabe uliopo miongoni mwa washirika wa Dkt Ruto kuhusu kiongozi anayefaa kuwa mgombea-mwenza wake.

Wanasema washirika wake wakuu wanahofia huenda wanasiasa wanaotangaza kujiunga na kundi hilo wakawa tisho kwao.

“Siasa zilizopo zinasukumwa na ubabe uliopo kuhusu kiongozi anayepaswa kuwa mgombea-mwenza wa Dkt Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Wanahisi wamehimili mawimbi ambayo mrengo huo umekuwa ukipitia, hivyo wanapaswa ‘kuzawadiwa’ kwa kutohama,” asema Bw Wycliffe Muga ambaye ni mdadisi wa masuala ya siasa.

Imeibuka kuwa moja ya makubaliano yaliyopo kati ya Dkt Ruto na viongozi wa Mlima Kenya ni kuwa lazima awatengee nafasi hiyo.

Baadhi ya viongozi wanaopigiwa upatu kupewa nafasi hiyo ni Bw Gachagua, mbunge Moses Kuria (Gatundu Kusini), aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri kati ya wengine.

Hata hivyo, Bi Wamuchomba anasema uamuzi wao ulichochewa na mwelekeo wa kisiasa ulio katika ukanda huo.

“Maamuzi yetu hayapaswi kumtishia yeyote. Yamechochewa na mwelekeo ambao wananchi wetu wamechukua,” akasema Bi Wamucomba.

Wachanganuzi wanasema kuwa kibarua kikubwa alicho nacho Dkt Ruto ni kuhakikisha kuwa taharuki miongoni mwa viongozi hao haigeuki kuwa hali itakayozua migawanyiko ya kisiasa.

“Ikiwa analenga kuibuka mshindi kwenye uchaguzi ujao, lazima Dkt Ruto afanye kila awezalo kuhakikisha washirika wake wamedumisha umoja,” asema Dkt Godfrey Sang’, ambaye ni mdadisi wa siasa.

You can share this post!

Ahadi ya Omanyala kuzoa medali kwenye mbio za mita 100...

Shirika laangazia dhuluma, mahangaiko ya wasichana kipindi...