• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Raila amezea mate OKA

Raila amezea mate OKA

DERICK LUVEGA na ANTHONY KITIMO

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga ataungana tena na vinara wenzake wa NASA ili kuunda muungano mpya utakaomwezesha kushinda urais mwaka wa 2022.

Bw Odinga alidokeza hilo siku chache baada ya vyama vya Amani National Alliance (ANC), Wiper na ODM kutangaza kujiondoa kwenye muungano wa NASA uliobuniwa kabla ya uchaguzi wa 2017.

Bw Odinga aliyekuwa akizungumza jana katika mazishi ya Ashura Bakari, 46, mke wa Naibu Gavana wa Vihiga, Dkt Patrick Saisi, alisema ataanza mazungumzo na viongozi wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA) – unaojumuisha vyama vya Wiper, ANC, Ford Kenya na Kanu –baada ya kukutana na viongozi wa maeneo mbalimbali nchini.

Bw Odinga alisema NASA tayari imevunjika na atajiunga na muungano mwingine kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Bw Odinga alionekana kumjibu kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka ambaye Jumamosi aliwataka viongozi wa vyama tanzu vya NASA iliyovunjwa waungane tena katika muungano wa OKA.

Bw Musyoka aliyekuwa akizungumza jijini Mombasa alisema mzozo kuhusu ugavi wa fedha ambao ulisambaratisha NASA, haufai kuwa kikwazo kwao kuungana tena.

Chama cha ODM kimekubali kutoa Sh153 milioni kwa vyama tanzu vya NASA; ANC kinachoongozwa na Musalia Mudavadi, Wiper, Ford Kenya kilicho chini ya Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula na Chama Cha Mashinani (CCM) cha aliyekuwa Gavana wa Bomet Isaac Ruto.

Wiper itapokea Sh70.4 milioni, ANC Sh43.8 milioni, Ford-Kenya Sh36.04 milioni na CCM Sh3.08 milioni.

Endapo vyama hivyo vitaitikia wito wa Bw Musyoka, hii itakuwa mara ya tatu kwa Bw Musyoka, Bw Mudavadi, na Bw Wetang’ula kubuni muungano kabla ya uchaguzi mkuu.

Jana, Bw Odinga alisema kwamba wiki hii atakutana na viongozi kutoka Nyanza kwa lengo la kujitafutia uungwaji mkono.Jumamosi, waziri huyo mkuu wa zamani atakutana na viongozi kutoka eneo la Magharibi mjini Kakamega na kisha kuelekea Pwani, Ukambani, Kaskazini Mashariki, Bonde la Ufa, Mlima Kenya na hatimaye jijini Nairobi.

“Baada ya mikutano hiyo, nitaanza kufanya mazungumzo na viongozi wa muungano wa OKA.“Tulijiondoa NASA lakini hatua hiyo haimaanishi kwamba hatuwezi kufanya kazi pamoja. Tutashirikiana katika siku za usoni,” akasema Bw Odinga.

Washirika wa Bw Mudavadi waliokuwepo jana mazishini, hata hivyo, walimtaka Bw Odinga kushirikiana na kinara wa ANC ili kushinda urais mwaka ujao.

Wabunge Bw Omboko Milemba (Emuhaya), Bi Beatrice Adagala (Vihiga) na Bw Alfred Agoi (Sabatia) walielezea masikitiko yao kufuatia kuporomoka kwa muungano wa Nasa.

Bw Milemba alimwambia Bw Odinga kuwa yeye na viongozi wenzake wa NASA watafaulu tu kuunda serikali mwaka ujao iwapo wataunda muungano thabiti.

“Sisi tutaunga mkono Bw Odinga kupitia kwa kiongozi wetu Bw Mudavadi,” akasema Bw Milemba.

Bw Agoi alisema kuwa Bw Odinga atafanikiwa kupata kura katika eneo la Mlima Kenya iwapo ataungana na Bw Mudavadi.

“Mudavadi ana mikakati tosha ya kupata kura nyingi katika eneo la Mlima Kenya. Nilisoma magazetini kwamba Raila hana mikakati yoyote ya kupata kura katika eneo la Mlima Kenya. Raila ajiunge na OKA ili twende pamoja 2022,” akasema Bw Agoi.

Mbunge huyo alionya kuwa viongozi wa NASA wakikosa kuungana wataaibishwa na Naibu wa Rais William Ruto 2022.

Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya alionya kuwa jamii ya Waluhya haitaweza kuingia Ikulu 2022 bila kuungana na viongozi wa maeneo mengine.

Alisema kuwa viongozi wa Magharibi wanafaa kuanza kuzungumza na viongozi wa maeneo jirani kama vile Nyanza na Bonde la Ufa ili kutimiza ndoto ya kushinda urais mwaka ujao.

“Mimi sina shida na wito wa jamii ya Waluhya kuungana. Hata kama tutaungana, tunahitaji jirani zetu. Tuanzie Nyanza na Nandi,” akasema Bw Oparanya.

You can share this post!

AFC Leopards youth yateleza ligi ya NWRL

Kwa sasa Raila ndiye Naibu Rais – Murkomen