• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 6:55 PM
Kalonzo amrai Shahbal arejee chamani Wiper

Kalonzo amrai Shahbal arejee chamani Wiper

Na ANTHONY KITIMO

KIONGOZI wa Chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka amemrushia ndoano mfanyabiashara Suleiman Shahbal ambaye amepanga kuwania ugavana Mombasa mwaka ujao.

Akiwa katika ziara mjini humo wikendi, Bw Musyoka alisema chama chake kingependa wanachama waliokihama warudi ili washirikiane kukiimarisha.

Hayo yalitokea siku chache baada ya Taifa Leo kufichua kuwa Bw Shahbal bado hajajiunga rasmi na Chama cha ODM jinsi alivyokusudia.

Bw Musyoka alitoa wito huo pia kwa aliyekuwa Seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar ambaye hushirikiana na Naibu Rais William Ruto chini ya Chama cha United Democratic Alliance (UDA) anapopanga kuwania ugavana.

“Shahbal alikuwa mwaniaji wetu wa ugavana, tunamwomba arudi katika Wiper ili tuwe na chama cha nguvu. Wito wetu unamwendea pia Bw Omar ambaye amejiunga na chama kisicho na uongozi bora,” akasema Bw Musyoka.

Bw Shahbal alikuwa mwanachama wa Wiper ambacho alitumia kuwania ugavana 2013, lakini akahamia Jubilee wakati wa uchaguzi wa 2017.

Mapema mwezi uliopita, alitangaza kuhama Jubilee na kupanga kujiunga na ODM ambacho anatumai kutumia kushindania kiti cha Hassan Joho atakayekamilisha kipindi chake cha pili cha ugavana mwaka ujao.

Hata hivyo, wiki iliyopita ilifichuka kuwa bado hajajiunga rasmi na ODM.Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Shahbal alisema angali anaendeleza mpango wa kuhamia ODM lakini kuna masuala anayostahili kukamilisha kwa afisi ya msajili wa vyama.

Endapo atahamia chama hicho kinachoongozwa na Bw Raila Odinga, mfanyabiashara huyo atapigania tikiti ya kuwania ugavana dhidi ya Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir.

Kiti hicho cha ugavana kimemvutia pia Mbunge wa Kisauni, Bw Ali Mbogo ambaye ni mwanachama wa Wiper.Ijapokuwa Bw Mbogo huegemea upande wa Dkt Ruto, alihudhuria mkutano wa kiongozi wa chama chake wikendi.Wakati huo huo,

Bw Musyoka ameashiria kufa moyo kuhusu marekebisho ya katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI).Hivi majuzi, Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga wakizungumza katika hafla tofauti walisisitiza kuwa malengo ya BBI yatafanikishwa.

Mpango huo ulisitishwa baada ya Mahakama Kuu kuamua ulikuwa haramu, na waasisi wake wakakata rufaa ambayo ingali mahakamani.

“Hata ingawa BBI imepitwa na muda, tunavyoona jinsi baadhi ya viongozi wanazungumzia kuinua uchumi wa taifa kutoka kwa wananchi wa ngazi za chini inayonyesha kutakuwa na mijadala ya kisiasa ambayo itahakikisha pia madiwani wamefadhiliwa vyema ili kupanua uchumi kwa Wakenya walio mashinani,” akasema.

Bw Musyoka alikuwa amezuru Mombasa kwa maandalizi ya uchaguzi ujao ambapo alirai wanachama waliohama warudi.

Alisema chama hicho kitaendeleza mikutano kadhaa eneo la Pwani wiki hii kabla kuelekea kaunti nyinginezo nchini.

Vyama tofauti vya kitaifa vimekuwa vikikita kambi eneo hilo katika miezi ya hivi majuzi kujitafutia umaarufu huku juhudi za baadhi ya viongozi kuunda muungqno wa vyama vya Pwani zikizidi kuchelewa.

You can share this post!

WANTO WARUI: Tutahadhari kuhusu corona Kidato cha Kwanza...

Kamishna aagiza wauzaji wa barakoa feki wanaswe