• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
CECIL ODONGO: ODM isiingie mkataba kipofu kama wa Nasa

CECIL ODONGO: ODM isiingie mkataba kipofu kama wa Nasa

Na CECIL ODONGO

BAADA ya kujiondoa katika muungano wa NASA, ODM inafaa kujihadhari na kumakinika kabla ya kuingia mkataba wa kisiasa na chama chochote kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.

Hii ni kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ambayo itaizuia kushiriki malumbano na umaarufu wake kuvinufaisha vyama vingine hasa kifedha jinsi ilivyo kwa sasa.

ODM wiki jana ililazimika kunywea na kugawa Sh308 milioni ilizopata kutoka kwa wizara ya Fedha baada ya kuingia katika muungano na vyama vinne vikuu katika uchaguzi uliopita.

Kuelekea uchaguzi Mkuu wa 2017, chama hicho kiliingia muafaka wa kisiasa na Wiper yake Kalonzo Musyoka, Ford Kenya ya Moses Wetang’ula, ANC ya Musalia Mudavadi na Chama cha Mashinani (CCM) cha Isaac Ruto.

Vinara hao wanne walishirikiana na kuendesha kampeni kali ya kumvumisha Kinara wa ODM Raila Odinga.

Hata hivyo, Bw Odinga alibwagwa na Rais Uhuru Kenyatta japo wawili hao walizika tofauti zao na kuanza kufanya kazi pamoja mnamo 2018.

Baada ya vuta nikuvute tangu 2017, ODM iilisalia na Sh187.9 milioni huku Wiper ikipata Sh70.4 milioni, ANC ikajizolea Sh43.8 milioni, Ford Kenya Sh36 milioni na Sh3 milioni kwa CCM.

Japo, vyama hivi tanzu vilitaka mgao sawa na ODM, uongozi wa chama hicho ulishikilia kuwa ulipata fedha hizo kutokana na hesabu za kura na viti ilivyoshinda vya ugavana, useneta na ubunge wala si urais kwa kuwa NASA ilisusia duru ya pili ya kura ya kumenyana na Rais Uhuru Kenyatta.

Hata hivyo, ni wazi kwamba vyama hivi vimekuwa mzigo mkubwa kwa ODM iwapo matokeo ya kura ya 2017 yatazingatiwa.

Ili kuepuka hili, ODM inafaa kumakinikia mkataba inaposaka muungano mpya na isisitize kwamba pesa zitagawanywa kutokana na idadi ya viti ambavyo kila chama kitashinda badala ya kura za urais.

Hii ni kwa sababu vyama vikishinda viti vingi ndani ya muungano, inakuwa rahisi kusukuma ajenda zake nyingi bungeni na serikalini.

Kwanza, inashangaza kuwa Wiper ambayo kwa sasa ina kiti kimoja cha ugavana imekuwa ikiishinikiza ODM iipe mgao sawa wa kifedha.

Chama hicho kilishindwa kupata hata kiti cha ugavana katika kaunti za Machakos na Kitui huku kikilazimika kushirikiana na chama cha Muungano chake Prof Kivutha Kibwana katika siasa za Makueni.

Hata Prof Kibwana tayari amekosana na uongozi wa Wiper huku Gavana wa Taita Taveta Granton Samboja naye akionekana kuegemea upande wa ODM licha ya kuchaguliwa kwa tiketi ya Wiper.

Pia Jubilee ilipata viti vingi Ukambani na kuipa ushindani mkali Wiper katika ngome yake ya kisiasa.

Vyama vya ANC, Wiper na Ford Kenya na CCM vina jumla ya wabunge ambao idadi yao hata haifikii 40 ilhali vinataka mgao sawa na ODM ambayo ina wabunge 72.

Kwa kuwa huenda vyama hivi vikaungana tena hata baada ya ODM kusalia kivyake na washirika wake kuhamia OKA, chama hicho kinafaa kimakinike na kisisitizie mkataba ambao unazingatia viti vya uwakilishi badala tu ya kura za urais.Kwa hivyo, ANC, Ford Kenya, Wiper na Kanu kupitia muungano wao mpya wa OKA zijizatiti na zidhihirishe weledi wao kisiasa kwa kushinda viti vingi 2022 ili kuwaonyesha wakosoaji kuwa hawakuwa wakinufaika tu kwa jasho la ODM.

Hiyo itasaidia kila chama kujizatiti ili kishinde viti vingi, hali ambayo itarahisisha uwezekano wa muungano wao kubuni serikali.

Mbali na hayo, vyama vyetu havifai kutegemea mgao wa fedha kutoka kwa mfuko wa vyama vya kisiasa ila vinafaa viwe na wanachama wengi na kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kuvipa mapato.

Hii itapunguza mizozo ya kifedha ya kila mara ndani ya muungano.Inasikitisha kuwa baadhi ya viongozi wa vyama vya kisiasa wanadai kuwa wana ushawishi ilhali vyama vyao hata havina afisi katika maeneobunge mbalimbali nchini.

You can share this post!

Wataalam wa maabara kizimbani kwa vyeti feki

MARY WANGARI: Tujihadhari hili zimwi la matumizi ya pufya...