• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Sababu zilizofanya chama cha Jubilee kusambaratika

Sababu zilizofanya chama cha Jubilee kusambaratika

Na JUSTUS OCHIENG

CHAMA tawala cha Jubilee kimepoteza umaarufu wake baada ya kuangushwa kwenye chaguzi ndogo katika ngome zake hivi majuzi huku uhasama katika ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto ukisemekana kuzorotesha hali hata zaidi.

Chama hicho, kilichobuniwa 2016 baada ya kuunganishwa kwa vyama 12, kimekosa umaarufu ilhali kilishinda viti vya kuchaguliwa katika kaunti 41 kati ya 47 katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Jubilee ilishinda viti 171 katika Bunge la Kitaifa; viti 140 katika jumla ya maeneo bunge 290, viti 25 miongoni mwa wabunge wawakilishi wa kaunti na wabunge sita kati ya wabunge 12 maalum.

Chama hiki kilisalia na wabunge 62 pekee ili kutimiwa kiwango cha thuluthi mbili ya idadi jumla ya wabunge, 349, katika bunge la kitaifa.Chama hicho kinachoongozwa na Rais Kenyatta pia kilishinda viti 25 vya ugavana na kina maseneta 34 kati ya maseneta wote 67.

25 kati ya maseneta hao ni wale waliochaguliwa na 10 ni wale walioteuliwa.Licha ya taswira hii inayoashiria chama chenye nguvu, mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu ujao, Jubilee imegeuka mahame.

Wadadisi wa kisiasa wanasema hali ilianza kuenda mrama katika Jubilee baada tu ya Rais Kenyatta na naibu wake Dkt Ruto kulishwa kiapo kuanza kuhudumu muhula wa pili.

Vile vile, chama kiliendelea kuporomoka zaidi baada ya Rais Kenyatta kuridhiana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga mnamo Machi 18, 2018.

Baada ya maridhiano hayo, maarufu kama handisheki, wandani wa Dkt Ruto maarufu kama Tangatanga, waliingiwa na woga na kuanza kusaka chama mbadala kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2022.

“Mvutano katika Jubilee unatokana na haja ya Rais Kenyatta kucheza siasa zitakazomwezesha kuacha sifa nzuri atakapostaafu huku naibu wake akiendeleza siasa za urithi. Hii ndio maana wanasiasa hao wawili wanavuta pande tofauti,” anasema Bw Dismas Mokua, mchanganuzi wa masuala ya siasa.

Anasema kuwa, ilivyo sasa, Jubilee sio chombo bora kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2022 kwa sababu kinahusishwa na usimamizi mbaya wa kiuchumi na utepetevu.

“Wakenya wanateseka kwa sababu ya utawala wa Uhuru na Ruto ambao chini ya Jubilee umechangia uchumi kuzorota, gharama ya maisha kupanda na mapato yao kudidimia.

“Kwa hivyo, sio jambo la kushangaza kwamba Naibu Rais Dkt Ruto ameteua chama kipya cha United Democratic Alliance (UDA) kwa sababu anataka kujitenga na makosa ya Jubilee,” Bw Mokua anaongeza.

Jubilee, anaongeza, inawakumbusha Wakenya kuhusu machungu ya kiuchumi na hivyo sio chama ambacho mwanasiasa yeyote angetaka kukitumia kuwania urais 2022.

You can share this post!

Mzozo wa nyadhifa ODM watishia kuangusha chama

Kumzuilia Ruto ni sawa na jinsi Miguna alihangaishwa, adai...