• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Rais Suluhu, SADC waomboleza kifo cha waziri wa ulinzi wa TZ

Rais Suluhu, SADC waomboleza kifo cha waziri wa ulinzi wa TZ

NA AFP

RAIS Samia Suluhu Hassan jana alituma risala za rambirambi kufuatia kifo cha Waziri wa Ulinzi na Huduma za Kitaifa, Elias Kwandikwa.

Waziri huyo ambaye alikuwa mbunge wa Ushetu katika eneo la Shinyanga, aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 55 mnamo Jumatatu usiku katika hospitali moja jijini Dar es Salaam.

Kupitia taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Afisi ya Rais, Jaffar Haniu, Suluhu alihuzunishwa na habari kuhusu kifo cha Kwandikwa.

“Tumempoteza mtu muhimu ambaye mchango wake katika kuhudumia umma hautasahaulika. “Alikuwa kiongozi imara aliyetekeleza majukumu yake kulingana na sheria na kanuni,” ilisema taarifa ya ofisi hiyo bila kutaja kiini cha kifo chake waziri huyo.

Suluhu alituma ujumbe wa kumfariji Mkuu wa Kikosi cha Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo.Waziri huyo ndiye afisa wa kwanza mkuu nchini Tanzania kufariki tangu Rais Suluhu akabidhiwe mamlaka mnamo Machi, kufuatia kifo cha mtangulizi wake John Magufuli.

Kifo cha Kwandikwa ni pigo kuu kwa serikali wakati huu Tanzania inapojitahidi kulinda ardhi yake, tangu kuzuka kwa machafuko nchini Msumbiji.

Marehemu alizaliwa Julai 1, 1966 na aliwahi kuhudumu pia kama naibu waziri katika wizara za huduma ya umma, usafiri na mawasiliano tangu Oktoba 2017.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Stargomena Tax, alituma pia rambirambi zake.

Alimsifia Kwandikwa kama atakayekumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika kukomesha wanamgambo wenye itikadi kali maeneo ya Cabo Delgado nchini Msumbiji.

“Tumepokea kwa huzuni kuu habari kuhusu kifo chake. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake pema peponi,” alisema kupitia ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.

You can share this post!

Matumaini ya kufufuka kwa Mumias yaimarika

Viongozi wa OKA wataka Moi ataliki Uhuru ajiunge na...