• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 9:12 AM
CORONA: Mombasa yapiga marufuku matibabu ya nyumbani

CORONA: Mombasa yapiga marufuku matibabu ya nyumbani

Na WINNIE ATIENO

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa imepiga marufuku matibabu ya nyumbani kwa wagonjwa wanaougua Covid-19 baada ya kufichuka kuwa kuna watu walioanza kutoa huduma za wagonjwa mahututi nyumbani.

Wahudumu wa afya walilaumiwa kwa kuanza kutoa nyumbani huduma ambazo kwa kawaida hutolewa katika vyumba vya matibabu ya dharura hospitalini (ICU).

“Tumegundua kuwa baadhi ya wahudumu wetu wa afya wanatoa huduma za ICU nyumbani kwa wagonjwa mahututi ndio maana tumeanza kupokea visa vingi vya corona miongoni mwao (wahudumu wa afya),” alisema Bi Pauline Oginga ambaye ni afisa mkuu wa afya ya umma Kaunti ya Mombasa.

Serikali kuu ilianza huduma za matibabu ya nyumbani kwa wagonjwa wa virusi vya corona wasiokuwa na dalili zinazohatarisha maisha yao mwaka uliopita ili kupunguza msongamano na kukabiliana na maambukizi.

“Kuna taratibu mwafaka zilizofaa kufuatwa ili mgonjwa aruhusiwe kutibiwa nyumbani au kama anafaa kulazwa hospitalini, iwe ya umma au ile ya kibinafsi. Tumegundua wahudumu wa afya wameanza kupatikana na corona kwa sababu ni wao ambao wanatoa huduma za ICU nyumbani kwa wagonjwa,” akasema Bi Oginga.

Hata hivyo, haijabainika wazi wale watakaopatikana wameambukizwa virusi hivyo watalazwa wapi, kwani serikali ya kaunti ilisema vitanda vilivyotengewa wagonjwa wa Covid-19 katika vituo vya afya vimejaa.

Mwenyekiti wa kamati inayosimamia masuala ya Covid-19 Mombasa, Bw Gilbert Kitiyo alionya kwa watu wanaojitengenezea vyumba vya mahututi nyumbani wakome akisisitiza kuwa ni uvunjaji wa sheria.

Akiongea kwenye kikao cha wanahabari katika afisi ya Gavana Hassan Joho hapo jana, Bw Kitiyo na kamati yake walisema kaunti hiyo imeanza kurekodi virusi vingi vya corona kwa hivyo itabidi wakazi watahadhari kwa kufuata kanuni zote za kuepusha maambukizi.

Bi Oginga alisema kuna taratibu mwafaka wa matibabu ya wagonjwa wa corona nyumbani.

Kamati hiyo pia ilisema itabuni kamati ndogo katika Kaunti Ndogo za Changamwe, Jomvu, Kisauni, Mvita, Likoni na Nyali ili kuanza misako ya wanaokiuka maagizo ya afya hasa hoteli, baa, magari ya umma na maduka makuu.

“Wale waaopatikana wamekiuka wafungiwe biashara zao,” alisisitiza Bw Kitiyo.

Idadi ya maambukizi imekuwa ikiongezeka kwa kasi kitaifa huku Mombasa ikiwa miongoni mwa kaunti ambazo huwa na idadi kubwa ya maambukizi kwa mujibu wa takwimu ambazo hutolewa na Wizara ya Afya.

You can share this post!

Siwezi kufanya kazi na Raila, Ruto asema

Dhuluma za kisaikolojia zinavyawatesa wanandoa kipindi cha...