• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Vigezo muhimu vya kuzingatia kufanikisha kilimo cha blue berries

Vigezo muhimu vya kuzingatia kufanikisha kilimo cha blue berries

Na SAMMY WAWERU

UHABA wa matunda ya blue berries nchini unaendelea kushuhudiwa, kutokana na idadi ya chini mno ya wakulima wanaoyakuza.

Kakuzi PlC, ni kati ya kampuni zinazoyalima nchini. Kampuni na watu wachache wanaoyakuza wakitajwa, Wilson Ndung’u hatakosa kuwa kwenye orodha.

Amekumbatia kilimo cha matunda haya adimu eneo la Limuru Kaunti ya Kiambu na Lavington, jijini Nairobi. Licha ya uhaba kuwepo, anasema Kenya ina uwezo kuyazalisha. Ina hali bora ya anga na pia udongo wenye rutuba.

Muhimu kulingana na mkulima huyu, ni kuwa na mbegu au miche, chanzo cha maji ya kutosha na safi na kuelewa kuyapanda na matunzo.

Kiunga cha Ndung’u eneo la Lavington kikiwa ni cha kuzalisha miche, anaorodhesha mbinu kadhaa za upanzi wa blue berries.

“Kuna upanzi wa mbegu, zinazoagizwa kutoka nje ya nchi. Mbinu hii, huchukua hadi kipindi cha miaka mitano kuanza kuzalisha matunda.

“Nyingine, yanapoendelea kutunda, matawi yake yanaweza kutumika kwa njia ya kupandikiza (grafting), na huchukua miaka miwili pekee kuanza kuzalisha,” afafanua.

Mkulima huyu amekumbatia mfumo wa air layering. Aidha, ni mfumo wa kutumia matawi ya blue berries, yanafungwa kwa kutumia Sphagnum moss (malighafi asilia, inayosifiwa kuhifadhi kiwango cha maji au unyevunyevu), na kuyatunzia kwenye vyungu, ambapo yakichipuka yanapaswa kupandwa.

Kulingana na mkulima huyu, huanza kuchana maua na kutunda pindi baada ya upanzi, akikadiria kuwa baada ya miezi minne hivi.

“Kwa kutumia mfumo huu, mimea michanga inapohamishiwa shambani wakati ikianza kukua haishuhudii msongo wa ‘mawazo’,” asema.

Mbinu nyingine ni ya tissue culture (uzalishaji wa miche iliyoimarishwa kiteknolojia), Ndung’u akisema anashirikiana kwa karibu na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Mimea na Uimarishaji Mifugo (Karlo), kupata miche ya hadhi ya juu.

“Karlo inanisaidia kuzalisha. Ninalenga kupata karibu miche 100, 000,” adokeza mwasisi huyu wa The Lavington Herbs Farm.

Kwa mujibu wa maelezo yake, blue berries hufanya bora zinapokuzwa kwenye udongo wenye asidi, hususan changarawe iliyochanganywa na mbolea za mboji/hai. Uchachu wa asidi unaopendekezwa uwe kati ya pH 4.2 hadi 5.5.

“Ni muhimu kupogoa matawi na kupulizia dawa dhidi ya wadudu na magonjwa haja inapoibuka,” Ndung’u ashauri.

Anasema amekumbatia mfumo wa kilimohai. Blue berries huhitaji maji mengi na safi, changamoto anayosema inaendelea kumtatiza kwani hutegemea yale ya mvua.

Kero nyingine ni matunda kushambuliwa na nyuni, hasa vipande vya shamba ambavyo hana viunga vya neti.

“Visa vichache vya wadudu aina ya vidukari, vithiripi, nzige na panzi hushuhudiwa. Magonjwa si kikwazo, hasa mkulima anapozingatia mbinu bora kitaalamu,” asema mtaalamu Vincent Ochieng kutoka Karlo.

You can share this post!

Mkuzaji stadi wa matikitimaji Pwani anayetaka vijana...

Jiandaeni kwa kiangazi na njaa, shirika laonya