• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
ODM yaponda ‘usuhuba’ wa Ruto, Museveni

ODM yaponda ‘usuhuba’ wa Ruto, Museveni

Na CHARLES WASONGA

KUNDI la wabunge wa ODM limemshtumu Naibu Rais William Ruto kwa kukiri kuwa na uhusiano na chama tawala nchini Uganda, National Resistance Movement (NRM).

Wakiongozwa na mwenyekiti wa ODM John Mbadi na Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed wabunge hao walidai Dkt Ruto anapanga kutumia NRM kusababisha machafuko nchini endapo atapoteza katika uchaguzi wa urais 2022.

Wabunge hao pia walidai kuwa urafiki kati ya Dkt Ruto na Rais wa Uganda Yoweri Museveni unalenga kumsaidia Naibu huyo wa Rais kutumia mbinu ‘chafu’ kuingia mamlakani.

“Tunafahamu fika jinsi huyo rafiki wake aliingia mamlakani na namna ambavyo amehujumu demokrasia na haki za kibinamu nchini Uganda akiwa mamlakani kwa zaidi ya miongoni mitatu. Ruto anataka kuleta udikteta kama huo nchini Kenya,’ Bw Junet akasema, akisoma taarifa kwa niaba ya wenzake 10 katika majengo ya bunge, Nairobi.

“Hatutaki kuingilia siasa za ndani za mataifa mengine. Lakini tunataka kueleza waziwazi kwamba hatuhitaji kukopa mienendo ya kisiasa kutoka mataifa hayo ambayo yanaweza kuleta machafuko katika taifa letu,” Bw Junet akaongeza.

Huku wakionya Wakenya dhidi ya uongozi wa Dkt Ruto, wabunge hao walielezea hofu kwamba Naibu huyo wa Rais atakwamilia mamlakani endapo atachaguliwa kumrithi bosi wake Rais Uhuru Kenyatta.

‘”wa kukumbatia NRM na sera zake za kiimla, zinazokiuka haki za kibinadamu na uhuru wa kujieleza, Dkt Ruto amefichua kuwa maisha yatakuwa magumu zaidi chini ya uongozi wake. Pia ameonyesha kuwa akipata mamlaka hataachilia anavyofanya rafiki yake katika taifa hilo,’ Bw Junet ambaye ni kiranja wa wachache bungeni akaeleza.

Kwa upande wake, Bw Mbadi alisema ni kinaya kwamba Dkt Ruto anadai amebuni mfumo wa kiuchumi ambao utaleta ustawi nchini ilhali anawapeleka wawekezaji katika nchi jirani ya Uganda.

“Huu mfumo wake wa kuchochea ukuaji wa kiuchumi kutoka ngazi za mashinani hautasaidia Kenya ikiwa ataendelea kuwapeleka wawekezaji nje. Mbona hakumshauri mwekezaji kutoka Uturuki kuwekeza hapa Kenya?’ akauliza mbunge huyo wa Suba Kusini.

Akiongea jana asubuhi katika runinga ya Inooro TV, Dkt Ruto alikariri kuwa Rais Museveni ni rafiki yake na ‘rafiki wa Kenya’.

“Ni kweli kwamba Rais wa Uganda Yoweri Museveni ni rafiki. Lakini yeye pia ni rafiki wa Wakenya wote ikizingatiwa kuwa Ugannda ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa Kenya,” Dkt Ruto akasema.

“Nimewahi kumfanyia kampeni. Na viongozi wote wa Nasa pia wamewahi kumfanyia kampeni. Sasa ikiwa yeye ni rafiki wa wote mbona kuna shida kubwa ikiwa Naibu Rais anamtembeleo kiongozi kama huyo?” akauliza.

Dkt Ruto pia alimtetea raia wa Uturuki kwa jina Harun Aydin ambaye alikuwa miongoni mwa watu ambao waliratibiwa kusafiri pamoja naye katika ziara ya Uganda iliyotibuka Jumatatu.

“Huyu ni mfanyabiashara na mwekezaji. Yeye sio gaidi au mhalifu wa aina yoyote inavyodaiwa na watu wengine,” akaeleza.

Dkt Ruto alizuiwa kuondoka kuondoka nchini kusafiri hadi Uganda kwa kile kilichosemekana kama kukosa idhini kutoka kwa afisi ya rais.

Naibu Rais alilazimika kukaa katika uwanja wa ndege wa Wilson mwa muda wa saa tano, lakini mwishowe maafisa wa uhamiaji walikataa kumruhusu kusafiri.

Hata hivyo, wabunge Oscar Sudi (Kapseret), Benjamin Tayari (Kinango) na Ndindi Njoro (Kiharu) pamoja na wafanyabiashara wandani wake waliruhusiwa kusafiri hadi Uganda.

You can share this post!

‘Mulmulwas’ atangaza vita vya kumpokonya...

Madiwani Kisumu walaumiwa kwa ziara ya Tanzania