• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Messi kuondoka Barcelona

Messi kuondoka Barcelona

Na MASHIRIKA

BARCELONA wamethibitisha kwamba nyota Lionel Messi hatasalia kambini mwao muhula huu kwa sababu ya “changamoto za kifedha na za kimuundo”.

Messi, 34, amekuwa mchezaji huru tangu Julai 1, 2021 wakati ambapo mkataba wake na Barcelona ulitamatika rasmi.

Ingawa alihiari kusalia ugani Camp Nou huku akidumishwa kwa mshahara uliopunguzwa kwa asilimia 50, mpango huo ulitegemea iwapo Barcelona wangeuza “idadi nzuri” ya wachezaji ili kumudu ujira mpya wa Messi.

“Pande zote mbili zinasikitika kwamba matamanio ya mchezaji huyo na waajiri wake hayatatimizwa hatimaye,” ikasema sehemu ya taarifa ya Barcelona.

Kwa mujibu wa Barcelona, Messi alitarajiwa kurefusha kipindi chake cha miaka 21 kambini mwa kikosi hicho kwa kutia saini mkataba mpya mnamo Agosti 5, 2021.

Licha ya Messi kukubali kusalia Barcelona hadi 2026, vinara wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) walishikilia kwamba klabu hiyo ilikuwa na ulazima wa kupunguza gharama yao ya matumizi ya fedha kabla ya Messi na wanasoka wengine wapya wa Barcelona kusajiliwa kwa ajili ya kampeni za msimu wa 2021-22.

Messi ndiye mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Barcelona. Amefungia kikosi hicho jumla ya mabao 672 na kunyanyua mataji 10 ya La Liga, manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na saba ya Copa del Rey. Messi ametawazwa pia mshindi wa taji la Ballon d’Or mara sita. Tuzo hiyo hutolewa kwa mwanasoka bora zaidi duniani kila mwaka.

Kumdumisha Messi uwanjani Camp Nou ni suala ambalo lilipewa kipaumbele na rais mpya wa Barcelona, Joan Laporta. Hata hivyo, mustakabali wa nyota huyo kitaaluma umevurugwa na hali tete ya kifedha kambini mwa Barcelona.

Messi ambaye ni miongoni mwa wanasoka bora zaidi duniani kwa sasa huenda akayoyomea Paris St-Germain au Manchester City ambako ataungana na kocha wake wa zamani kambini mwa Barcelona, Pep Guardiola.

Kuna uwezekano pia wa Messi kutua Amerika kunogesha kivumbi cha Major League Soccer (MLS) ambacho sogora huyo raia wa Argentina amekuwa akitamani sana kusakata.

Tangazo la Barcelona kwamba Messi yuko huru kutafuta hifadhi mpya kwingineko linatolewa mwaka mmoja baada ya sogora huyo kutaka Barcelona kumwachilia ajiunge na kikosi chochote kingine bila ada yoyote mwishoni mwa msimu wa 2019-20.

Siku chache baadaye, ilibainika kwamba hakukuwa na klabu yoyote iliyokuwa radhi kuweka mezani Sh97.3 bilioni ili kufanikisha uhamisho wa Messi kwa mujibu wa kipengele fulani kwenye mkataba wake.

Messi aliingia katika sajili rasmi ya Barcelona akiwa na umri wa miaka 13 mnamo 2000 baada ya kuagana na kikosi cha Newell’s Old Boys. Aliwajibishwa na Barcelona katika kikosi cha watu wazima kwa mara ya kwanza mnamo 2004 akiwa na umri wa miaka 16.

Tangu wakati huo, amechezeshwa na Barcelona mara 778 na akafunga mabao 672, yakiwemo 120 ya UEFA na 474 katika La Liga.

Ametwaa taji la European Golden Shoe mara sita baada ya kuibuka mfungaji bora zaidi katika soka ya bara Ulaya.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Spurs wataka Man-City iwape Sh24.9 bilioni kwa ajili ya...

Shahbal hatimaye aingia ODM