• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Kenya na TZ kurahisisha upimaji corona

Kenya na TZ kurahisisha upimaji corona

Na WINNIE ONYANDO

HUENDA visa vya wasafiri kulazimishwa kupima upya corona mpakani mwa Kenya na Tanzania vikakoma baada ya serikali hizo mbili kufanya mashauriano.

Jana, mawaziri wa afya Mutahi Kagwe (Kenya) na Dorothy Gwajima (Tanzania) walikubaliana kuingilia kati kutatua suala hilo.

Hii ni kutokana na malalamishi yaliyotolewa na madereva na wafanyabiashara, hasa wanaotumia mpaka wa Namanga. Wasafiri hao wanadai kuchukua muda mrefu wakisubiri wakaguliwe mizigo na kupimwa upya corona.

Bi Gwajima aliahidi kuwa wale ambao wamepata chanjo au kupimwa corona hawatahitajika kupimwa tena mpakani.

“Ikiwa mtu atakuwa amepokea chanjo katika nchi moja, hatalazimishwa kupimwa tena. Hii ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma zitakazowapendeza,” alisema Bi Gwajima.

Mawaziri hao walisema kuwa hatua hiyo itakuwa njia ya kuimarisha sekta ya biashara katika nchi hizo mbili na hata kudumisha uhusiano mwema kati ya wananchi.

Waliwahimiza wananchi kushirikiana na serikali katika kupambana na virusi vya corona.“Ni jukumu la kila mmoja kujilinda ndipo tutaangamiza janga hili. Tukishirikiana kitaaluma, kimawazo na kibinafsi, basi hakuna kitakachotushinda,” alisema Bw Kagwe.

Aliwaonya wananchi wanaokiuka kanuni za kudhibiti maambukizi kuwa watachukuliwa hatua.“Idadi ya maambukizi inaendelea kupanda huku wengi wakifa kutokana na ugonjwa huu. Tusipojitahadhari, tutaendelea kupoteza wapendwa wetu,” akasema Bw Kagwe.

Alitoa mfano wa familia moja katika Kaunti ya Kiambu iliyowapoteza watatu watatu kutokana na janga hilo.Alizitaka serikali za kaunti kuhakikisha kuwa hospitali zote zina oksijeni ya kutosha.

Waziri Kagwe aliwataka walimu wahakikishe wamepata chanjo dhidi ya corona, ili kuzuia maambukizi miongoni mwa wanafunzi.

Kaunti ya Murang’a imefunga Makao yake Makuu kwa siku kumi na nne kutokana na ongezeko la idadi ya maambukizi.

Afisa wa Afya wa kaunti hiyo, Bw James Mbai alisema kuwa wafanyikazi wa serikali katika kaunti hiyo wameambukizwa virusi hivyo, jambo lililowalazimisha kufunga ofisi zao.

Hayo yakijiri, jana wizara ya Afya ilitangaza kupanda kwa kiwango cha maambukizi nchini kufika asilimia 17.Watu 1,571 waliambukizwa virusi hivyo huku 32 wakifa.

Kati ya hao, watatu walikuwa ndani ya saa 24 ilihali 29 ni vifo vilivyoripotiwa kuchelewa.

You can share this post!

Uhuru ajaza nafasi nne za makamishna wa IEBC

Nitagura Jubilee kwa hiari ila si kwa kushurutishwa –...