• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 1:14 PM
Hatari wakazi ‘wakisusia’ madaraja ya barabara kuu

Hatari wakazi ‘wakisusia’ madaraja ya barabara kuu

Na WACHIRA MWANGI

WAKAZI wa jiji la Mombasa ‘wamesusia’ madaraja yaliyojengwa kwa kutumia mamilioni ya fedha ili kulinda maisha yao.

Madaraja hayo yalijengwa na serikali ya kitaifa pamoja na ya kaunti kuwaepusha na ajali zinazotokea wanapovuka barabara kuu katika jimbo hilo.

Lakini wakazi wamesusia madaraja ya Shimanzi, Buxton na Kongowea na badala yake wanahatarisha maisha yao kwa kwa kutumia maisha yao na kutumia barabara iliyo na msongamono mkubwa wa magari.

Madaraja hayo sasa yamekuwa makazi ya watoto wa mitaani, maarufu chokoraa, maficho ya wezi na maeneo ya kibiashara kwa wachuuzi.

Mkuu wa trafiki eneo la Pwani, Bw Peter Maina, alionya kuwa wanaotembea kwa miguu wanahatarisha maisha yao kwa kutumia barabara kuu na zenye misongamano ya magari.

“Madaraja hayo ya waenda kwa miguu hayatumiki ipasavyo. Wakazi hawaoni umuhimu wake na wanavuka barabara kuu bila kujali hatari ya kugongwa na magari,” Bw Maina aliambia Taifa Leo.

Aliongeza: “Polisi hawezi kumlazimisha mtu mzima kutumia daraja. Ni jukumu la kila mmoja kutii kanuni za trafiki kwa kufanya kinachohitajika.”

Mkurugenzi Mkuu wa Uchukuzi katika Kaunti ya Mombasa, Bw Albert Keno, naye alisikitika kwamba kanuni hiyo ya kutumia madaraja kama kivuko, inakiukwa kiholela kote nchini.

Bw Keno aliongeza kuwa watu wengi hupuuza kutumia vivukio hivyo hata ikiwa kuna misongamano barabarani.

“Madaraja ya waenda miguu yamewekwa kwa ajili ya usalama wa wananchi, sio kama maonyesho. Kumekuwa na misongamano mikubwa ya magari katika barabara zilikojengwa madaraja ya Fidel Odinga sokoni Kongowea, Buxton na Shimanzi,” akasema Bw Keno.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa serikali itahakikisha kuwa madaraja yametumika ipasavyo na yasiwe tu maeneo ya wachuuzi.

Kutimiza hilo, serikali itaanzisha zoezi la kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia madaraja hayo.

You can share this post!

Maandalizi ya kura ya maamuzi yashika kasi

Hisia mseto Ezekiel Mutua akitimuliwa kutoka kwa bodi ya...