• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 3:34 PM
Wakosoa Magoha kutosajili shule

Wakosoa Magoha kutosajili shule

Na SAMWEL OWINO

WAZIRI wa Elimu, Prof George Magoha amekosolewa na wabunge kuhusu agizo lake la kusitisha usajili wa shule mpya.

Wabunge walisema kuwa hatua hiyo itaathiri sekta ya elimu.Walidai kuwa hatua hiyo inakinzana na sera ya serikali kuhakikisha kuwa asilimia 100 ya wanafunzi wanaofanya Mtihani wa Darasa la Nane (KCSE) wanajiunga na shule za sekondari.

Hayo yanajiri shule za sekondari ziking’ang’ana kusajili wanafunzi wote 1,179,192 waliofanya mtihani mapema mwaka huu.

Nafasi zilizoachwa na watahiniwa wa Kidato cha Nne mapema mwaka huu ni 747,161. Hiyo inamaanisha kuwa zaidi ya wanafunzi 400,000 watakosa nafasi au watalazimika kusongamana shuleni na kuwaweka katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona.

“Sera ya kusitisha usajili wa shule mpya inafaa kuondolewa. Tunatarajia watoto wetu waende wapi baada ya kumaliza shule za Msingi ikiwa sekondari zimejaa,” akasema Kiranja wa Wengi Bungeni, Emmanuel Wangwe.

Mbunge wa Endebess, Bw Robert Pukose, alisema kuwa usajili wa shule mpya haufai kuonyesha upendeleo wa aina yoyote.

Alisema kuwa kila mtoto ana haki ya kusomea shule anayoitaka, hivyo usajili wa shule mpya ni njia mojawapo ya kuwapa watoto uwezo wa kuchagua shule wanayoipenda.

“Wizara inafaa kuondoa sera ya kusitishwa kwa usajili wa shule mpya. Katika eneobunge langu, kuna shule mbili mpya zilizojengwa kwa pesa ya maendeleo ya jimbo (CDF) na hawana walimu walioajirwa na serikali,” akasema Bw Pukose.

Bw Pukose alipinga sera hiyo akidai kuwa itafungia nje shule mpya zinazojengwa nchini.Wizara ya Elimu ilisitisha usajili wa shule mpya mnamo Juni, 15, 2021.

Sera hiyo ilisainiwa na Katibu wa Wizara ya Elimu, Julius Jwan, na kusambaziwa maafisa wa elimu wa kaunti zote 47.

“Hii ni kuwaarifu kuwa usajili wa shule mpya umesitishwa. Mchakato huo utaendelea baada ya mikakati mipya kuwekwa na mkurugenzi wa uhakikisho wa ubora na viwango vya masomo,” taarifa ulisoma.

Bw Jwan alisema kuwa walipokea orodha ndefu ya shule zinazotaka kusajiliwa kutoka kwa wakuu wanaosimamia shule kwenye kaunti mbalimbali.

Wizara ya elimu ilisitisha usajili wa shule mpya huku ikisema kuwa shughuli hiyo itarejelewa baada ya maafisa wanaohusika kuweka kanuni mpya.

Kamati hiyo inakumbwa na tatizo la ukosefu wa vifaa vya kutosha vya kuendesha shughuli yao, jambo linaloathiri mgao na matumizi ya rasilimali za umma.Wabunge wanatarajiwa kukutana na Bw Magoha ili kujadiliana kuhusu sera hiyo.

Waziri Magoha atayajibu maswali mbalimbali ya wabunge kuhusiana na masuala ya elimu na sera aliyoitoa kuhusiana na usitishaji wa usajili wa shule mpya.

Mwezi uliopita, Prof Magoha alisema kuwa serikali imeanza mchakato wa kufunga shule zilizo na idadi ndogo ya wanafunzi –hatua ambayo imekosolewa vikali.

Prof Magoha alisema kuwa kuna baadhi ya shule nchini zilizo na idadi ya chini ya wanafunzi 20 na zimekuwa zikipokea fedha kutoka kwa serikali.

You can share this post!

Shule yakosa kupata wanafunzi wa kidato cha kwanza

Museveni afokea Raila