• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Museveni afokea Raila

Museveni afokea Raila

Na LEONARD ONYANGO

CHAMA tawala nchini Uganda, National Resistance Movement (NRM), kinachoongozwa na Rais Yoweri Museveni kimeshutumu vikali ODM chini ya Raila Odinga kwa kudai kuwa kinalenga kushirikiana na Naibu wa Rais William Ruto kuzua machafuko humu nchini.

Katibu Mkuu wa NRM Richard Todwong jana alisema kuwa Rais Museveni hana nia ya kuingilia uchaguzi wa Kenya kumwezesha Dkt Ruto kumrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022.

Kupitia barua yake, Bw Todwong alionekana kumshambulia mkurugenzi wa mbunge wa Suna Junet Mohamed licha ya taarifa ya kukashifu NRM Jumatano ilitolewa na wabunge kadhaa wa ODM.

“Ninakuandikia kuhusiana na kauli chafu ambayo wewe pamoja na wenzako mlitoa kuhusiana na chama cha NRM na kumkosea heshima Rais Museveni.

“Matamshi hayo labda yalitokana na tofauti zenu za kisiasa nchini Kenya. Tunaamini kuwa kauli yenu sio msimamo wa chama cha ODM,” akasema Bw Bw Todwong.

Jumatatu, Naibu wa Rais Ruto alizuiliwa kusafiri kuelekea nchini Uganda kutokana na kigezo kwamba hakupata idhini kutoka kwa Rais Kenyatta.

Baadaye, mbunge wa Kapseret Oscar Sudi alikiri kuwa Dkt Ruto analenga kujumuisha washauri wa siasa wa Rais Museveni katika kikosi chake cha kampeni anapojiandaa kuwania urais 2022.

Bw Sudi aliambia Taifa Leo kuwa walienda Uganda kujifunza kutoka kwa chama NRM ambacho kimekuwa mamlakani kwa miaka 35 chini ya Rais Museveni.

Kundi la wabunge wa ODM, Jumatano, walishutumu Dkt Ruto kwa kukiri kuwa na uhusiano wa karibu na chama cha NRM.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa ODM John Mbadi na Bw Mohamed amabaye pia ni mkurugenzi wa uchaguzi wa chama hicho, wabunge hao walidai Dkt Ruto anapanga kutumia NRM kusababisha machafuko nchini endapo atapoteza katika uchaguzi wa urais 2022.

Wabunge hao pia walidai kuwa urafiki kati ya Dkt Ruto na Rais wa Uganda Yoweri Museveni unalenga kumsaidia Naibu huyo wa Rais kutumia mbinu ‘chafu’ kuingia mamlakani.

“Tunafahamu fika jinsi huyo rafiki wake aliingia mamlakani na namna ambavyo amehujumu demokrasia na haki za kibinamu nchini Uganda akiwa mamlakani kwa zaidi ya miongoni mitatu. Ruto anataka kuleta udikteta kama huo nchini Kenya,’” Bw Junet akasema, akisoma taarifa kwa niaba ya wenzake 10 katika majengo ya bunge, Nairobi.

Kauli hiyo ilionekana kukera viongozi wa NRM ambao jana walisema kuwa chama hicho kimekuwa na rekodi njema katika haki za kibinadamu.

“Mnasema kwamba chama cha NRM hakifai kuigwa, je, nadhani mnakumbuka ni nini kilisababisha ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007/2008 ambapo watu zaidi ya watu 1,000 walifariki ndani ya siku chache.

“NRM imeweza kuongoza Uganda kwa miaka 35 kwa sababu ya kuendeleza haki za kibinadamu na kupigania amani,” akasema Bw Todwong.

Katibu Mkuu wa NRM alipuuzilia mbali madai kwamba nchini Uganda hakuna demokrasia huku akisema kuwa kila kijiji nchini kinaongozwa na viongozi waliochaguliwa na wananchi kupitia vyama mbalimbali.

“Rais wetu mliyemtusi amechaguliwa na raia wa Uganda kwa njia ya kidemokrasia kutokana na maono yake,” akasema.

Bw Todwong alisema kuwa Uganda ina vituo vya redio 300 na runinga 50 ‘hivyo madai kwamba nchini Uganda hakuna uhuru wa vyombo vya habari hazina mashiko’.

Alisema kuwa tofauti na Kenya, Uganda haingozwi na siasa za ukabila bali wameungana.

“Ripoti ya hivi karibuni ilionyesha kwamba Uganda ndilo taifa lenye watu wenye furaha zaidi katika ukanda huu. Hiyo ndiyo maana wakimbizi, wakiwemo raia wa Kenya wanakimbilia nchini Uganda,” akadai.

Kiongozi wa ODM Bw Odinga na Rais Museveni wamekuwa na tofauti kwa muda mrefu.

You can share this post!

Wakosoa Magoha kutosajili shule

Kibicho: Tutaweka kamera za siri Gikomba kudhibiti mikasa...