• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
Shahbal ‘avuka kisiki’ katika urithi wa Joho

Shahbal ‘avuka kisiki’ katika urithi wa Joho

Na ANTHONY KITIMO

Mfanyabiashara wa Mombasa, Suleiman Shahbal, ameanza mikakati ya kumrithi Gavana wa Mombasa Hassan Joho, siku chache baada ya msajili wa vyama ya kisiasa kumruhusu kujiunga na chama cha ODM.

Bw Shahbal aliyejiuzulu kama mwanachama wa chama Jubilee kabla ya kujiunga rasmi na ODM, Ijumaa alifanya mkutano wake wa kwanza wa kisiasa na madiwani 21 wa bunge la kaunti ya Mombasa.

Kwenye mkutano huo uliofanyika katika Bahari Hotel mjini Mombasa, Bw Shahbal aliahidi kukutana na viongozi tofauti katika juhudi zake za kutafuta uungwaji mkono kuanzia mashinani.

“Tumevuka kisiki cha kwanza ambacho kilikuwa kuruhusiwa kujiunga na ODM jinsi wafuasi wangu wengi waliniomba kufanya. Wiki hii nilijiunga rasmi kama mwanachama wa maisha wa ODM baada ya kulipa ada ya Sh20,000 na sasa kilichobaki ni kualika kila mtu kushirikiana nami,” alisema Bw Shahbal.

Aliongeza: “Baadhi ya watu wananiuliza kwa nini ninazunguka na kiongozi wa ODM Raila Odinga, ninataka kuwaambia kwamba kila mtu anahitaji kuungwa mkono na viongozi wengine, hauwezi kufanya kazi peke yako lakini sitafuti kuidhinishwa kwa kuwa siogopi mchujo,” alisema Bw Shahbal.

Mfanyabiashara huyo pia alisema kwamba mbali na kukutana na viongozi, anatarajia kupata wafuasi kupitia mpango wake wa Gumzo Na Shahbal ambao amekuwa akikutana ana kwa ana na wananchi mashinani kwa mazungumzo.

Katika mpango huu analenga wadi zote 30 za Mombasa.Baada ya kujiunga na ODM, Shahbal sasa ataanza kampeni yake kugombea ugavana Kaunti ya Mombasa kama mwanachama wa chama hicho.

Bw Shahbal atamenyana na mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir ambaye amekuwa akidai mfanyabiashara huyo ni mgeni ambaye amekuwa akihamahama vyama vya kisiasa.

Bw Nassir amekuwa na matumaini kwamba atashinda mchujo wa ODM kwa kuwa amekuwa mwaminifu kwa chama hicho ambacho amekuwa mwanachama kwa mwongo mmoja.

Bw Nassir pia amekuwa akisema hatarajii kuidhinishwa na kiongozi wa chama na kwamba anachohitaji ni baraka na kwamba ni wapigakura watakaoamua ikiwa anafaa kwa kiti hicho.

“Ushirikiano wangu wa karibu na Bw Odinga na Bw Joho hauhusiani na kutaka kuidhinishwa na kutembea naye ni kwa manufaa ya umoja wa chama pekee. Ninachotaka ni baraka zao lakini ni wapigakura watakaoniidhinisha,” alisema.

You can share this post!

Kibicho: Tutaweka kamera za siri Gikomba kudhibiti mikasa...

CAVB yathibitisha Kenya imeingia Kombe la Voliboli Afrika