• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
WARUI: Mfumo wa CBC ni mzigo kutokana na ughali wa vifaa

WARUI: Mfumo wa CBC ni mzigo kutokana na ughali wa vifaa

Na WANTO WARUI

HUKU ratiba ya elimu ikiendelea kusukuma wazazi haraka haraka bila mapumziko, wazazi walio na wanafunzi wanaosoma mfumo mpya wa CBC wameanza kuhisi uzito mapema.

Masomo ya CBC yanaelekea kuwa mengi zaidi ya yale ya 8-4-4, hivyo basi mzigo kuwa mzito zaidi.

Wazazi wenye wanafunzi wanaosoma katika Gredi ya 4 na 5 wamejipata pabaya katika ununuzi wa vitabu. Gredi za 4 na 5 zina masomo yapatayo 13 katika silabasi zao na walimu wametoa orodha ya vitabu vya masomo hayo yote kwa wazazi ili vinunuliwe. Shule nyingi hasa zile za kibinafsi zinadai mwanafunzi awe na vitabu vya kusoma visivyopungua kumi. Gharama ya vitabu hivi iko juu sana hasa ikichukuliwa kuwa wakati huu wananchi wengi wana shida kubwa ya pesa kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19.

Bei ya kitabu kimoja haipungui sh450 kwa hivyo akinunua vitabu kumi tu anatumia takriban sh5,000.

Aidha kuna vitabu vya kuandikia, kalamu, sare za shule, viatu na mahitaji mengine ya kusomea. Mzazi anajipata akitumia pesa nyingi sana kugharimia masomo haya. Mmojawapo wa wazazi katika duka moja la kuuzia vitabu alifichua hali imekuwa ngumu sana kwa kuwa ana watoto watatu wa Gredi ya 5, mwengine Gredi ya 3 na mmoja sekondari na ameshindwa kuwanunulia vitabu vyote kutokana na ughali wake na ukosefu wa pesa.

Karibu kila familia inalia. Shule nazo hazijatoa mwelekeo ufaao wa vitabu ili kuwe na nafuu kwa wazazi kubadilishana vitabu badala ya kununua vipya kila mwaka.

Kutozoeleka na kukosa mwelekeo ufaao katika mfumo mpya wa CBC aidha kumesababisha kuchanganyikiwa kwa walimu na wazazi. Shule nyingi zinabadilisha orodha ya vitabu kila mwaka zikijaribu kutafuta vilivyo bora. Kampuni za uchapishaji wa vitabu nazo ziko mbioni kuingia sokoni kila kukicha. Soko la vitabu limejaa vitabu vya kila aina.

Shule za sekondari nazo hazijaachwa nyuma. Kilio ni hicho hicho tu cha vitabu na karo ya shule.

Wazazi wanaowapeleka wana wao sekondari kujiunga na kidato cha kwanza wamejipata wakihangaika kwa kukosa kuridhisha mahitaji ya shule.

Ingawa serikali imepunguzia wazazi mzigo wa kulipa karo, bado hakuna afueni kutokana na pigo kubwa la biashara na kudorora kwa biashara na ukosefu wa kazi nyingi kutokana na ugonjwa huu wa Covid-19.

Njia mbadala ambazo wazazi wanakimbilia za kupokea msaada wa basari ambao ni bahati nasibu. Mzigo wa elimu umekuwa mkubwa sana na serikali inafaa kuangalia upya sera zake za elimu ili kurahisisha maisha!

You can share this post!

ONYANGO: Nauli zipunguzwe kufuatia agizo la kujaza abiria...

Polo aporwa na kisura ‘malaika’