• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Makundi 10 ya wafanyabiashara Thika yapokea mkopo wa Sh1.4 milioni

Makundi 10 ya wafanyabiashara Thika yapokea mkopo wa Sh1.4 milioni

Na LAWRENCE ONGARO

VIKUNDI 10 vya wafanyabiashara vimenufaika na mkopo ya Sh1.4 milioni ili kujiendeleza zaidi.

Fedha hizo zimetolewa na serikali kupitia kwa hazina ya kuondoa ufukara yaani Poverty Eradication Fund ili kuwapa mwelekeo wa kujiendeleza kibiashara.

Afisa wa idara ya Shirika la maendeleo kaunti ndogo ya Thika Magharibi, Bi Mercy Kinoti, alieleza kuwa kila kikundi kinajumuisha kati ya watu 10 na 20 ambao wanatarajia kuendesha biashara zao kwa pamoja.

Alisema vikundi hivyo vilipokea kati ya Sh50,000 hadi Sh250,000 ili kupanua biashara zao mashinani.

“Kwanza kabla ya kutoa kiwango hicho kwa vikundi hivyo, tunawahamasisha kwa kuwapa mawaidha kuhusiana na biashara,” alifafanua Bi Kinoti.

Wanufaika walishauriwa kurejesha hela hizo chini ya kipindi cha miezi 12 ili pia vikundi vingine viweze kunufaika na mkopo huo.

Wote waliopokea mkopo huo walishauriwa kutumia fedha hizo kwa makini ili ziweze kuwanufaisha pamoja na familia zao.

Bi Kinoti alihimiza vikundi vingi vijitokeze na kujisajili kwa afisi za serikali ili pia wanachama wao nao waweze kunufaika pakubwa na mikopo hiyo.

Wengi waliofika kupokea fedha hizo walipongeza juhudi za serikali za kuwajali wafanyabiashara wa viwango vya chini huku wakitaka waongezwe fedha zaidi.

Naibu kamishna wa Thika Magharibi Bw Mbogo Mathioya aliyehudhuria hafla hiyo, aliwahimiza waliopokea fedha hizo kuwa makini wasishawishike kuingilia anasa.

“Hizo fedha ni muhimu kwa matumizi yenu ya kibiashara, na kwa hivyo msiingilie anasa,” aliwashauri Bw Mathioya.

Aliwataka wahusika wawe mstari wa mbele kulipa deni hilo kwa wakati ufaao ili vikundi vingine pia viweze kunufaika.

Wote waliopokea mikopo hiyo walipongeza juhudi za serikali kuona ya kwamba imeinia hali yao ya maisha na kuinua biashara zao.

Bw Joshua Maina kutoka kijiji cha Kiandutu alisema “tangu janga la Covid-19 lilipotuvamia hapa nchini watu wengi wameishi katika hali ngumu ya maisha.”

Lakini baada ya mikopo hiyo kutolewa rasmi na serikali hali ya maisha kwa wengi imebadilika.

“Sisi kama kikundi cha Tumaini Self Help Group tumenufaika pakubwa ambapo tunaiomba serikali izidi kusambaza mikopo hiyo kwa watu wengi vijijini,” alisema Bw Maina.

You can share this post!

Pigo Barcelona jeraha likitarajiwa kumweka nje Aguero kwa...

Mourinho aonyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi kati ya AS...