• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 PM
Familia zaidi ya 50 zapoteza nyumba zao kwenye mkasa wa moto

Familia zaidi ya 50 zapoteza nyumba zao kwenye mkasa wa moto

Na SAMMY KIMATU

MALI yenye thamani ya mamilioni ya pesa iliteketea usiku wa kuamkia Jumatatu katika kisa cha moto kwenye mtaa mmoja wa mabanda, Kaunti ya Nairobi.

Mkasa huo ulitokea katika eneo la Express katika mtaa wa mabanda wa Kayaba ulioko kaunti ndogo ya Starehe.

Aidha, zaidi ya familia 50 zilibakia bila makao baada ya nyumba zao kuteketea kwenye mkasa huo.

Chifu wa eneo hilo, Bw Charles Karanja alisema moto ulianzia katika nyumba moja kabla ya kuenea kwa kazi hadi nyumba jirani.

“Moto ulianza mwendo wa saa kumi na mbili kasorobo kutoka kwa nyumba moja kabla ya kuenea kwa kazi na kuteketeza nyumba zingine,” Chifu Karanja akasema.

Katika kisa hicho, moto ulienea hadi ukafikia yadi mbili zilizokuwa za biashara ya makaratasi ya plastiki, katoni na mapipa ya rangi.

Mmiliki wa stoo moja iliyokuwa na mali nyingi ya kuuza, Bw Charles Otieno Roba, alisema anakadiria hasara ya thamani ya zaidi ya Sh5 milioni.

“Nikihesabu hasara ya mali niliyopoteza katika kisa cha moto wa leo, sioni ikiwa chini ya Sh5 milioni,” Bw Otieno asema.

Mwathiriwa mwingine, Bw Eric Karume Njoka alisema kulingana na makali ya ndimi za moto, hangeweza kuokoa chochote.

Isitoshe, wakazi waliofika kusaidia kuzima moto walilazimika kutazama kwa mabali kufuatia milipuko ya mitungi na kemikali za mapipa ya rangi iliyoogofya.

“Milipuko ya mitungi ililazimisha kila mmoja wetu kukimbilia usalama wake kwa kuogopa. Wazimamoto walikuwa wakijaribu kupambana na moto lakini maji yalikuwa yakiisha kwa malori yao kila wakati wakiuzima moto,” Bw Roba akasema.

Hiki ni kisa cha tatu cha moto kuripotiwa kwa kipindi cha mwezi mmoja mtaani humo.

Kadhalika, polisi wameanzisha uchunguzi kubaini kilichosababisha moto ikizingatiwa kwamba hakuna stima katika mtaa huo kufuatia operesheni ya majuzi.

“Hatuna stima mtaani baada ya msako dhidi ya wanaounganisha stima kinyume cha cheria uliofanywa na polisi wakishirikiana na maafisa wa kampuni ya kusambaza stima nchini,” chifu Karanja akasema.

Mnamo Julai, moto mwingine uliteketeza nyumba 50 katika eneo la Budalangi lililo kwenye mtaa huo huku mtoto mmoja akinusurika kifo kwa tundu la sindano.

Katika mtaa wa mabanda wa Fuata-Nyayo kwenye tarafa ya South B, watu wawili walifariki baada ya kuteketea kiasi cha kutotambulika haraka.

Zaidi ya nyumba 130 ziliteketea wakati wa mkasa huo.

You can share this post!

Spurs wataka Lautaro Martinez wa Inter Milan ajaze pengo la...

Wakulima Kiambu wapokea hundi ya Sh39 milioni kupiga jeki...