• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
KINA CHA FIKIRA: Epuka kujipaka uchafu ndipo nzi wasikusumbue

KINA CHA FIKIRA: Epuka kujipaka uchafu ndipo nzi wasikusumbue

Na WALLAH BIN WALLAH

BABU yangu Mzee Majuto bin Kengemeka aliniambia zamani nilipokuwa kijana mchanga kwamba watu humchukia nzi -mdudu mdogo tu- na kumlaumu kuwa anaambukiza magonjwa mbalimbali kama vile kipindupindu, homa ya matumbo, ugonjwa wa macho na mengineyo.

Huo ni ukweli kabisa! Nzi ni mdudu hatari sana kwa afya ya wanadamu na wanyama! Lakini tujiulize nzi humfuata mtu au mnyama mwenye sifa na hulka gani?

Kwa hakika nzi hatui wala haendi mahali bila kuwapo na kitu au vitu vinavyomvutia kuenda kutua pale kama vile uchafu na uvundo!

Ukitaka kuwaepuka nzi ili wasikusumbue, uondoe uchafu! Ama uondoke mahali penye uvundo!

Ni kazi bure kupigana na nzi hata ukitumia marungu, mishale, nyundo, bunduki au mawe endapo umejipakaza uvundo au umekaa palipo na uchafu! Nzi watang’ang’ania pale pale! Watakusumbua tu mpaka ujisafishe uondoshe uchafu ubakie ukiwa safi!

Wahenga walisema kwamba, ‘Mwenye kidonda ndiye amwogopaye nzi.’ Mtu asiye na kidonda hashtuki hata akimwona nzi akitua mwilini pake kwa sababu hana jeraha ambalo nzi ataanza kung’ong’ona!

Kasoro zetu na uchafu wetu hutuletea matatizo makubwa maishani kisha tunaparamia kulalamika!

Katika kuyachunguza mambo utagundua kwamba wanyama wakubwa wote wa porini na nyumbani wana matatizo na mahangaiko makubwa bila utulivu! Chunguza uone! Kila wakati wanyama hao wanapotembea au wanapolala wana wasiwasi hawatulii kamwe! Watazame simba, nyati, ndovu, chui, ng’ombe, punda, nyumbu, pundamilia na wengineo. Kila wakati wanarusharusha na kutikisatikisa miguu yao, mikia yao na masikio yao kwa sababu wanasumbuliwa na wadudu hao wadogo waitwao nzi!

Nzi hung’ong’a na kuwang’ong’ona wanyama wakubwa hao kwa sababu wana vidonda na uchafu unaotafutwa na nzi. Wanyama hawanawi nyuso zao, hawaoshi macho yao, hawapigi miswaki baada ya kula! Hawasukutui vinywa vyao wala kusafisha masikio yao! Viungo vyao vyote hivyo vina uchafu unaowavutia nzi na kusababisha nzi kuwahujumu, kuwasumbua na kuwakera wanyama wakubwa!

Hayo ndiyo masaibu na madhila waliyo nayo wanyama wakubwa wasiojua kujisafisha kuondoa uchafu ili wasisumbuliwe na wadudu wadogo kama nzi!

Ndugu wapenzi, matatizo ya mwanadamu huletwa na mwanadamu mwenyewe! Chambilecho Profesa Ebrahim Hussein katika kitabu cha Kinjeketile kwamba, ‘Binadamu huzaa neno kisha neno likawa kubwa kumshinda binadamu aliyelizaa!’

Ni vizuri mtu ajitakase awe safi ili asije akateswa na kujutia makosa yake mwenyewe hatimaye aanze kuwalaumu nzi wadudu wadogo ambao wamefuata uchafu aliojipaka binadamu! Ondoa uchafu! Uwe safi! Ukiepuka kujipaka uchafu, nzi hawatakusumbua!

[email protected]

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: Hakuna kuathiriwa kabla ya tukio

WASONGA: Uadilifu ndicho kiungo muhimu uchaguzini wala si...