• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
WASONGA: Uadilifu ndicho kiungo muhimu uchaguzini wala si hela!

WASONGA: Uadilifu ndicho kiungo muhimu uchaguzini wala si hela!

Na CHARLES WASONGA

HUKU taifa likijiandaa kwa uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 9, 2022, maandalizi ya shughuli hiyo ya kitaifa ni muhimu zaidi kwani ndiyo yataamua ikiwa utafanikiwa au la.

Kiwango cha ufanisi wa shughuli hiyo kitakadiriwa kwa misingi ya ukubalifu wa matokeo ya uchaguzi huo unaotarajiwa kushuhudia ushindani mkubwa haswa katika kinyang’anyiro cha urais.

Hii ni kwa sababu Rais Uhuru Kenyatta atastaafu baada ya kukamilisha muhula wake wa pili na wa mwisho kwa mujibu wa Katiba.

Kivumbi kikali pia kitashuhudiwa katika kinyang’anyiro cha ugavana ikizingatiwa kuwa kiti hicho ndicho chenye ushawishi mkubwa katika ngazi za kaunti.

Joto jingi haswa litashamiri katika kaunti 23 ambazo magavana wazo wanahudumu kwa muhula wa pili na wa mwisho, na hivyo hawatakuwa kinyang’anyironi.

Ni kwa misingi hii ambapo nahisi macho ya Wakenya wote yataelekezwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ambayo ndiyo ina wajibu mkubwa wa kufanikisha maandalizi hayo.

Lakini ufanisi wa IEBC utategemea usaidizi mkubwa kutoka kwa serikali kuu, bunge, vyama vya kisiasa na raia kwa ujumla.

Licha ya changamoto kadha, haswa za kifedha ambazo IEBC inatarajiwa kukumbana nazo, tume hii isitumie sababu hizo kama kizingizio cha kufanya maandalizi chapwa yatayochangia kutoaminika kwa matokeo ya uchaguzi.

Itakumbukwa kwamba ghasia za baada ya chaguzi za 2007 na 2017 zilichangiwa pakubwa na utendakazi duni wa tume hiyo kuanzia awamu ya maandalizi, usimamizi wa upigaji kura hadi upeperushaji wa matokeo.

Mitambo

Kwa mfano, ilibainika kuwa baadhi ya mitambo ya kielektroniki iliyotumiwa kuendeshea uchaguzi wa 2017 ilikuwa duni na hivyo ikafeli kufanya kazi siku ya upigaji kura.

Katika uamuzi wake, Mahakama ya Juu iliamuru shughuli hiyo irejelewe na hivyo kumgharimu mlipa ushuru mabilioni ya fedha.

Tayari mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati ametangaza kuwa uchaguzi mkuu ujao utagharimu Sh40.9 bilioni na kwamba tume yake inakabiliwa na upungufu wa Sh14.5 bilioni kufikia bajeti yake.

Japo inatarajiwa kuwa Hazina Kuu inajizatiti kuziba pengo hilo kwa kuitengea tume hiyo fedha zaidi kupitia bajeti ya kitaifa ya mwaka wa kifedha wa 2022/2023 itakayosomwa mwezi wa Aprili 2022, sidhani kuwa fedha pekee ni suluhisho kwa tatizo la maandalizi ya uchaguzi.

Muhimu zaidi ni kuwa Bw Chebukati, makamishna wenzake na maafisa wa IEBC watahitaji kuongozwa na uadilifu katika uendeshaji wa shughuli za tume hiyo ili kuandikisha ufanisi katika uchaguzi huo.

Bw Chebukati na wenzake waelewe kuwa uadilifu kwa upande wao ni hitaji la kimsingi litakalowawezesha kuendesha uchaguzi huru na haki bali si uwepo wa fedha za kutosha.

You can share this post!

KINA CHA FIKIRA: Epuka kujipaka uchafu ndipo nzi...

Mawakili waliowakilisha Jumwa walia kuitiwa DCI