• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
TAHARIRI: Chanjo itasaidia wake wajawazito

TAHARIRI: Chanjo itasaidia wake wajawazito

KITENGO CHA UHARIRI

TANGU janga la Covid-19 libishe hodi duniani na nchini, kumekuwepo ripoti mbalimbali kuhusu athari na madhara ya ugonjwa huu ajinabi.

Kadri ya mpito wa wakati baadhi ya madai yaliyotolewa yamethibitishwa ama kuwa kweli au vinginevyo na wataalamu katika asasi za afya duniani.

Baadhi ya tetesi zilizoibuka punde tu baada ya chanjo za corona kuidhinishwa na kuanza kutumiwa kote duniani ni kwamba akina dada walikuwa katika hatari ya kudhuriwa endapo wangechanjwa.

Tetesi au madai haya yaliwatia uoga wanawake wengi na kuwafanya kuogopa kabisa kujitokeza kuchanjwa. Miongoni mwa wanawake, waliotiwa uoga zaidi ni wanawake wajawazito.

Hata hivyo, kadri ya mpito wa wakati takwimu zimeonyesha kwamba idadi ya wanawake wanaolazwa hospitalini kutokana na kuambukizwa corona ni wale ambao ni wajawazito.

Cha kutisha zaidi ni kwamba kundi hili la wanawake wanaolazwa wakiwa katika hali mbaya zaidi ni wale ambao hawajapata chanjo.

Kwa mujibu wa wataalamu, tukio hili si la kustaajabisha kwani kwa mujibu wa maumbile, mwanamke awapo mjamzito kinga yake hushuka.

Kwa hivyo itokeapo kwamba mtu kama huyu ataambukizwa corona, basi ina maana kwamba atakuwa katika hatari kubwa ikilinganishwa na watu wengine.

Ili kunusuru maisha ya baadhi ya wanawake wajawazito pamoja na watoto wao, madaktari wamekuwa wakilazimika kuwapa dawa zinazowawezesha kujifungua kabla ya wakati wao.

Hii inakuwa nafuu badala ya kuishia kuwapoteza wote wawili.

Kwa mintarafu na matukio haya, na hasa ikizingatiwa kwamba utafiti umefanywa na kubainika kwamba hakuna madhara yoyote ambayo yamejitokeza kwa wanawake wajawazito waliochanjwa, madaktari na wataalamu wa afya wanashauri kwamba kundi hili lihimizwe kuanza kupata chanjo kama njia mojawapo ya kuepuka hatari.

Chanjo itawawezesha akina mama hawa kuepuka madhara makali ya Covid-19 endapo wataambukizwa kinyume na sasa ambapo wengi wao huishia katika vyumba vya wagonjwa mahututi na baadhi ya kuishia kutegemea msaada wa oksijeni ya vipumulio.

You can share this post!

KASHESHE: Eti angeishia kuwa dereva wa trela

Kibarua cha Uhuru kupanga urithi OKA ikimkataa Raila