• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Karua aongoza Mlima kujipanga

Karua aongoza Mlima kujipanga

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha Narc Kenya, Martha Karua na wenzake wa Chama cha Kazi Moses Kuria na Mwangi Kiunjuri wa The Service Party of Kenya (TSP), wamemkosoa Rais Uhuru Kenyatta kwa kupuuza eneo la Mlima Kenya katika mipango ya siasa za urithi uchaguzi mkuu unapokaribia.

Walisema kwamba Rais Kenyatta hakualika viongozi wa eneo la Mlima Kenya kwenye mkutano wake na vinara wa vyama vya kisiasa katika Ikulu ya Mombasa, Jumanne wiki hii.

Kwenye mkutano huo, Rais Kenyatta alikutana na kiongozi wa ODM Raila Odinga, Kalonzo Musyoka wa Wiper, Musalia Mudavadi wa Amani National Congress (ANC), Moses Wetangula wa Ford Kenya, Gideon Moi wa Kanu na Wycliffe Oparanya ambaye ni naibu kiongozi wa ODM.

Inasemekana kuwa Rais Kenyatta aliwataka viongozi hao kuungana kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 ili kumshinda Naibu Rais William Ruto.

“Katika mkutano wa majuzi Mombasa, ni eneo la Mlima Kenya pekee ambalo halikuwakilishwa ilhali kuna eneo ambalo liliwakilishwa na viongozi watatu. Hii ni moja ya sababu zetu kuamua kuunda kundi la kuleta pamoja Mlima Kenya kuchukua mwelekeo wa pamoja,” walisema.

Hisia za viongozi hao ni kwamba Rais Kenyatta ataondoka mamlakani baada ya uchaguzi mkuu ujao na eneo hilo linafaa kuwa na kiongozi atakayewakilisha maslahi ya eneo la Mlima Kenya kwenye serikali ijayo.

Viongozi hao walisema kwamba nia yao ni kuunganisha eneo la Mlima Kenya kwa lengo la kuhakikisha maslahi yao yatawakilishwa kwenye serikali ijayo.

Kwa kufanya hivi, viongozi hao walisema wanalenga kongamano la tatu eneo la Limuru ambako eneo la Mlima Kenya litaamua mwelekeo wa kisiasa litakaochukua kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Jamii za Mlima Kenya chini ya mwavuli wa muungano wa Gema unaoleta pamoja Wagikuyu, Waembu na Wameru huwa zinakutana Limuru kuweka mikakati ya kisiasa na kuamua msemaji wao eneo hilo kabla ya uchaguzi mkuu.

“Tunatangaza kwamba Narc Kenya, The Service Party na Chama cha Kazi vimeunda kundi kwa lengo la kuhakikisha masuala na maslahi ya eneo la Mlima Kenya yatashughulikiwa. Tutapanua kundi hili kuhusisha wote walio na nia sawa,” walisema kwenye taarifa fupi iliyosomwa na Bi Karua jijini Nairobi.

Viongozi hao walisema kwamba wanatarajia kongamano la tatu la Limuru ndani ya miezi mitatu ijayo.

Kulingana na viongozi hao, mchakato ambao wameanzisha hautajumuisha wanasaisa pekee mbali utahusisha viongozi wengine wenye ushawishi wakiwemo viongozi wa kidini.

“Tunatambua kwamba maeneo mengine yanaendelea kuungana kwa lengo la kujipanga uchaguzi mkuu unapokaribia lakini sisi katika Mlima Kenya tumebaki nyuma,” alisema Bw Kiunjuri.

Wanasiasa hao walisema kwamba hawana nia ya kuvunja vyama vyao kuunda kimoja kuwasikilisha eneo hilo.

Vile Vile, Bw Kuria na Bw Kiunjuri walisema kwamba hawataunganisha vyama vyao na chama cha United Democratic Alliance cha Naibu Rais William Ruto inavyodaiwa na baadhi ya viongozi.

“Vyama vyote vilivyosajiliwa na msajili wa vyama ni vya kitaifa na kwamba hivyo vyetu sio vya kisiasa. Hatuna nia ya kuvunja vyama vyetu au kutaka vingine vivunjwe kwa kuwa kila kimoja kina malengo yake,” walisema.

Mbunge wa Kieni, Kanini Kega alikaribisha juhudi za wanasiasa hao akisema eneo la Mlima Kenya linahitaji kuungana kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

You can share this post!

Serikali yaendelea kuibua madai dhidi ya Harun Aydin

Raia wa Zambia kumjua mshindi wa urais wikendi hii