• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 3:34 PM
WASONGA: Serikali ikubali wazo la ODM uchumi ufunguliwe

WASONGA: Serikali ikubali wazo la ODM uchumi ufunguliwe

Na CHARLES WASONGA

SI kawaida yangu kukubaliana na nyingi za kauli na mapendekezo ya wanasiasa kutokana na imani kuwa hili ni tabaka la watu ambao aghalabu huweka mbele masilahi yao wala si ya raia wa kawaida.

Lakini kwa mara ya kwanza, nakubaliana na pendekezo la chama cha ODM kwamba serikali kuu ifungue nchi kwa kuondoa baadhi ya masharti ambayo yamkini yanadumaza juhudi za kufufua uchumi nchini.

Kupitia hoja iliyodhaminiwa na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sheriff Nassir, chama hicho haswa kinamtaka Rais Uhuru Kenyatta aondoe amri ya kutopatikana nje kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi alfajiri na marufuku ya usafiri wa usiku kwa magari ya uchukuzi wa umma.

Kwa mujibu wa ODM masharti hayo, ambayo yametekelezwa kuanzia Aprili mwaka wa 2020, yana madhara makubwa kwa uchumi ikilinganishwa na faida.

ODM inasema biashara nyingi haswa zile ambazo awali zilikuwa zikiendeshwa majira ya usiku, zitafufuka endapo amri ya kutopatikana nje usiku, almaarufu kafyu, itaondolewa na wafanyabiashara kuruhusiwa kuendesha shughuli zao kwa saa 24 ilivyokuwa awali.

Nakubaliana na wanasiasa hawa wa ODM kwamba ikiwa serikali imeruhusu magari ya uchukuzi wa umma kurejelea hali ya kawaida ya kubeba idadi kamili ya abiria, mbona magari haya yasiruhusiwe kuhudumu nyakati za usiku?

Pili, naunga pendekezo lao kwamba kile ambacho serikali kuu inapaswa kufanya wakati huu ni kuimarisha mikakati ya kuhakikisha kuwa raia wengi wanajitokeza kupewa chanjo ya kuwapa kinga dhidi ya Covid-19.

Kwa mfano, ni hatua ya busara kwamba serikali imeanzisha mpango wa utoaji chanjo kwa halaiki katika vituo vya magari ya uchukuzi na mitaa ya mashariki ya Nairobi.

Vile vile, serikali kupitia afisi ya Mkuu wa Utumishi wa Umma, Joseph Kinyua imetoa makataa kwa watumishi wa umma kupata angalau dozi ya kwanza ya chanjo kufikia Agosti 23, 2021 la sivyo wachukuliwe hatua za kinidhamu.

Serikali imechukua hatua hii kwani wakati huu Kenya haikabiliwi na uhaba wa dozi za chanjo aina ya AstraZeneca.

Imekuwa ikipokea chanjo hiyo kutoka mataifa fadhili.

Kwa mfano, ni juzi tu ambapo Wizara ya Afya ilipokea dozi 440,000 za aina hiyo ya chanjo kutoka Uingereza na inatarajia dozi nyingine 1,600,000 za chanjo aina ya Pfizer kutoka Amerika mwanzoni mwa juma lijalo.

Lakini sambamba na kuendeleza kampeni ya utoaji chanjo, serikali haina budi kutoa hamasisho kwa umma kuhusu usalama wa chanjo hiyo ili kuwavutia watu wengi kujitokeza wachanjwe.

Kuna porojo nyingi zinazosambazwa mitandaoni na katika majukwaa mengine kwamba chanjo ya AstraZeneca inasababisha madhara mbalimbali ya kiafya, kama vile utasa.

Kwa hivyo, ikizingatiwa kuwa wataalamu wanashikilia kuwa ugonjwa huu hautatokomezwa kabisa nchini na ulimwenguni hivi karibuni, Wakenya wanafaa kuzoea kuishi nao sawa na aina nyingine za homa.

Hii ndiyo maana naunga mkono wazo la ODM kwamba nchi ifunguliwe lakini raia waendelee kuzingatia masharti mengine yasiyo na madhara kwa uchumi wa nchi.

Hii ndio njia ya kipekee itakayoiwezesha Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) kufikia kiwango lengwa cha ukusanyaji ushuru cha Sh1.9 trilioni, kulingana na makadirio ya bajeti yam waka huu wa kifedha wa 2021/2022.

You can share this post!

Jamii yaiomba korti izuie operesheni za serikali Laikipia

Messi kusubiri zaidi kuchezea PSG baada ya kutambulishwa...