• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
Sitishwi na jeshi la wanaonipinga – Ruto

Sitishwi na jeshi la wanaonipinga – Ruto

Na JUSTUS OCHIENG

Naibu Rais William Ruto, jana alipuuza juhudi za Rais Uhuru Kenyatta za kuunganisha viongozi wa upinzani ili kumshinda kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Rais Kenyatta alikutanisha viongozi wa upinzani; Raila Odinga, Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka, Moses Wetang’ula na Gideon Moi huku ikisemekana aliwashawishi waungane kwa dhamira ya kumshinda Dkt Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Jana, Dkt Ruto alieleza kuwa hatishwi na muungano wa viongozi hao akisema kuwa wananchi wanataka huduma bora kutoka kwa viongozi wakuu nchini wala si mikutano inayoendelezwa na viongozi wanaopanga jinsi ya kugawana mamlaka.

Akihutubia wananchi mtaani Kawangware, Nairobi, baada ya kuhudhuria ibada katika Kanisa Katoliki la St Francis of Assisi – Gatina, Dkt Ruto alisema yuko tofauti na watu wachache wanaoendeleza siasa za kikabila na kuwa ataendelea kutetea maslahi ya watu wa tabaka la chini.

Dkt Ruto alisema ataunga mahasla kupinga mabadiliko ya katiba yanayolenga kuunda nyadhifa kwa minajili ya watu wachache.

Amekuwa akipinga mchakato wa kubadilisha katiba wa Mpango wa Maridhiano (BBI) ulioanzishwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga.

“Tunataka kuungana kwa lengo moja. Sote tulio mamlakani tunafaa kutafuta mbinu za kuwakilisha na kuunganisha Wakenya wote. Ninajua wale wanaume sita wanaelekea Naivasha kujitengea nyadhifa,” alisema.

Aliongeza, “Kuna Wakenya zaidi ya milioni 15 wanaohitaji kazi na nafasi ya kufanya biashara. Kwa maoni yangu, kinachofaa kupewa umuhimu katika taifa letu si viongozi kugawana nyadhifa na mamlaka lakini ni jinsi ya kubuni mabadiliko ya uchumi na kuunda nafasi za kazi na kutoa mazingira bora ya kila Mkenya kutumia talanta, nguvu na ujuzi wake kustawisha nchi,” alisema.

Aliwaambia viongozi wa kisiasa waliokutana na Rais Kenyatta kujiandaa kushindwa na mahsla kwenye uchaguzi wa mwaka ujao.

Hata hivyo, naibu kiongozi wa chama cha ANC, Ayub Savula alisema mkutano wa vinara wa One Kenya Alliance (OKA), Mombasa utaendelea leo licha ya madai ya Dkt Ruto.

You can share this post!

Lungu adai kura ya urais ilijaa dosari mpinzani akiongoza

Watatu wahofiwa kufariki katika ajali ya boti Lamu