• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
Wafuasi wa Ruto wamtongoza Kingi ajiunge na ‘mahasla’

Wafuasi wa Ruto wamtongoza Kingi ajiunge na ‘mahasla’

Na MAUREEN ONGALA

WANASIASA wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto, wameanza kumtongoza Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi ambaye anaendelea kuachwa pweke kisiasa.

Wiki iliyopita, Bw Kingi alipokonywa wadhifa wake wa uenyekiti wa ODM Kilifi baada ya mvutano wa muda mrefu kati yake na kiongozi wa chama, Bw Raila Odinga kuhusu msimamo wake wa kuunda chama cha Pwani.

Kabla ya hapo, Bw Kingi alikuwa ametengwa pia na wenzake ambao walianza naye safari ya kuleta umoja wa Wapwani, wakiwemo magavana Hassan Joho (Mombasa) na Salim Mvurya (Kwale), wabunge na viongozi wa vyama vitano ambavyo alitarajia vingeungana.

Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya ambaye ni mmoja wa wanasiasa walioasi ODM wakajiunga na Dkt Ruto eneo la Pwani, jana alisema mpango wa Bw Kingi kuunda chama kipya wakati huu hautafaa, na badala yake ajitolee kuunga mkono Chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Hii ni baada ya wandani wa Bw Kingi kusajili Chama cha Pamoja Alliance ambacho inasemekana atakitumia kuendeleza ajenda yake ya kupigania umoja wa Pwani kisiasa.

“Vyama vidogo havina nafasi ya kuleta maendeleo katika maeneo. Tunahitaji viongozi wetu waungane ili wawe na idadi ya kutosha ya kudhibiti maamuzi katika vyama vikubwa kama vile UDA,” akasema Bw Baya.

Bw Baya alikashifu ODM kwa kumpokonya gavana huyo wadhifa wake chamani na kusema chama hicho kimemsaliti sawa na jinsi ilivyomfanyia yeye na Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa.

“Ikiwa Raila alihisi kuwa mimi na Aisha tulimkaidi, angemwendea Kingi amwambie adhibiti uasi huo. Bw Odinga hakufanya hivyo. Alipuuza na kumtenga huku akitafuta ushauri kwa Gavana Joho,” akasema.

Aliongeza kuwa gavana alistahili kuheshimiwa ODM kwa sababu ya jinsi Kilifi ilivyochagua viongozi wote wa chama hicho 2017.

Mbunge wa Magarini, Bw Michael Kingi ambaye ni mwandani wa gavana, hata hivyo alipuuzilia mbali wito wa Bw Baya kutaka gavana ajiunge na UDA.

Huku akithibitisha kuna chama kilisajiliwa hivi majuzi, mbunge huyo alisema safari yao haiwezi kusitishwa wakati huu.

“Meli ilishang’oa nanga. Chama kitazinduliwa hata kama uchaguzi utakuwa umekaribia aje. Hakuna chochote cha kuhofia kwa sababu tunapigania wananchi wapate sauti itakayotetea masilahi yao,” akasema.

Viongozi wa vyama vya Shirikisho na Kadu-Asili ambavyo ni baina ya vitano vilivyonuiwa kuungana, waliambia Taifa Leo walikosa uaminifu kwa Gavana Kingi hasa baada ya kufichuliwa chama kinachohusishwa naye kilisajiliwa majuzi. Vyama vingine ni Republican Congress, Umoja Summit na Communist.

You can share this post!

Mbunge na abiria 30 wanusurika ndege ikiharibika angani

Corona ilivyohangaisha makahaba dhuluma zikiongezeka