• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 1:14 PM
Mutua na Lilian wafunikia kiini cha kutengana

Mutua na Lilian wafunikia kiini cha kutengana

Na BENSON MATHEKA

KUTENGANA kwa Gavana wa Machakos, Dkt Alfred Mutua na mkewe wa pili Lilian Nganga, kumezua mdahalo miongoni mwa Wakenya licha ya wawili hao kueleza kuwa walikubaliana kufanya hivyo kwa amani na hiari. Kulingana na Bi Lilian, ni yeye aliyeamua kumuacha Dkt Mutua.

“Upepo wa mabadiliko ulinisomba na miezi miwili iliyopita, niliamua kutamatisha uhusiano wangu wa miaka mingi na Dkt Alfred Mutua. Tulikuwa na wakati mzuri na nitashukuru Mungu daima kwa kutuunganisha,” Bi Lilian alisema kupitia mitandao ya kijamii kabla ya Dkt Mutua.

Kauli yake iliacha wengi wakijiuliza iwapo wawili hao walikuwa wameoana rasmi au ulikuwa uhusiano wa “njoo tuishi”.

Mjadala huo ulinonga kwa kuwa Dkt Mutua alipoteza mali ya mamilioni ya pesa kwa mkewe wa kwanza kwenye talaka ya kwanza na kwa kuwa Lilian ni mke wa pili kumuacha Dkt Mutua ndani ya miaka sita.

Mnamo 2015, Dkt Mutua alitalikiana na mkewe wa kwanza Dkt Josphine Thitu ambaye walikuwa wamezaa watoto watatu katika ndoa yao ya miaka 15.

Dkt Thitu aliambia mahakama katika kesi ya talaka kwamba Dkt Mutua alikuwa amehama nyumba waliyokuwa wakiishi katika eneo la Grivellea Road jiji Nairobi.

Alidai kwamba gavana huyo hakuwa ameishi katika nyumba hiyo tangu 2012. Mvutano ulizuka kuhusu mali ambayo Dkt Thitu alidai alifaa kumiliki na hatimaye akashinda mahakama ilipomkabidhi umiliki wa mali ya mamilioni ya pesa jijini Nairobi na kaunti za Machakos, Makueni na Kitui.

Talaka yao ilijiri baada ya Dkt Mutua kutangaza Lilian kuwa mkewe rasmi.Dkt Thitu alihamia Australia baada ya Dkt Mutua kumkabidhi Lilian majukumu ya mke wa gavana wa Kaunti ya Machakos.

Alipotangaza kutengana kwake na Dkt Mutua kupitia mitandao ya kijamii Jumapili, Lilian alijivua majukumu ya mke wa gavana Kaunti ya Machakos lakini akasema wataendelea kuwa marafiki na kutekeleza miradi yake kwa jamii.

Wawili hao wanamiliki hoteli ya A $ L mjini Machakos. Kulingana na Dkt Mutua, yeye na Lilian walikubali kutengana kwa amani na kwamba atamdumisha kama mshauri wake kwa kipindi cha mwaka mmoja kilichobaki akiwa gavana na anapoendelea na azma yake ya kugombea urais.

Alisema Lilian ambaye ni mwanamitindo wa zamani ataendelea kushiriki katika miradi yake.Dkt Mutua alimmiminia sifa Lilian akimtaja kama mwanamke mwerevu ambaye anatumai ataendelea kumfaa katika azma yake ya kugombea urais.

“Atabaki kuwa mshauri wa karibu ninapoendelea kusimamia Kaunti ya Machakos na kugombea urais kwa kuwa ninaamini werevu na moyo wake,” alisema Dkt Mutua na kukiri kwamba walikuwa wakitofautiana mara kwa mara katika uhusiano wao.

Baadhi ya Wakenya waliwasifu kwa kukubali kuvunja ndoa yao kwa amani, tofauti na ilipokuwa anatalikiana na Dkt Thitu.

Wawili hao hawakueleza sababu za kutengana na waliyokubaliana kuhusu mali lakini walisema kwamba wataendelea kuheshimiana. Mbali na hoteli ya A&L, haijulikani iwapo kuna mali nyingine wanayomiliki pamoja na thamani yake.

You can share this post!

Rutto aonya ugatuzi utafeli kabisa iwapo mbinu zake...

Nitawapa mashine za kisasa kuchapa kazi nikiingia Ikulu...