• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:04 PM
Chama cha Kiswahili shuleni Kitengela International ni mwale thabiti wa lugha

Chama cha Kiswahili shuleni Kitengela International ni mwale thabiti wa lugha

Na CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Kitengela International eneo la Syokimau, kilianzishwa kwa malengo ya kuchangia makuzi ya Kiswahili, kubadilisha mtazamo hasi wa wanafunzi kuhusu Kiswahili, kuzidisha maarifa ya utafiti katika Kiswahili na kuboresha matokeo ya KCPE Kiswahili.

Zaidi ya kuweka wazi umuhimu wa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi, chama hiki pia kiko mstari wa mbele kustawisha matumizi ya lugha shuleni na kupanua mawanda ya elimu katika nyanja nyinginezo zinazofungamana na Kiswahili.

Mbali na kuwa daraja la kuvusha watahiniwa katika masuala ya kiakademia, madhumuni mengine ya kuasisiwa kwa chama hiki ni kuwapa wanafunzi jukwaa mwafaka la kukuza vipaji vyao vya utambaji wa hadithi, uchoraji, uigizaji na utunzi wa mashairi.

Mnamo 2020, Kitengela International School Syokimau ilitia fora kwa mara nyingine katika KCPE chini ya uongozi wa Bw Andati (Mwalimu Mkuu).

Watahiniwa 26 kati ya 29 walipata zaidi ya alama 400 huku watatu waliosalia wakizoa kati ya alama 395 na 400. Shule iliandikisha alama wastani ya 410.38.

Baadhi ya walimu wanaosukuma gurudumu la Kiswahili shuleni humo chini ya Bw Gideon Mang’eli ambaye ni Mkuu wa Idara ni Stephen Muhanji, Winfridah Ayuma, Michael Wechune, Cyrus Musyoki, Janet Onyango, Cornel Range na Douglas Nyamamba.

Wengine ni Nicodemus Wambua, Zipporah Mukhwana, Juliah Kaminja na Janet Bonareri.Kwa mujibu wa Bw Mang’eli, wengi wa wanafunzi wao wanaothamini na kuchangamkia usomaji wa Taifa Leo, hudumisha umahiri wao katika lugha na mwishowe hukwangura alama za juu zaidi hata katika mitihani ya kitaifa ya KCPE.

Anaungama kuwa majaribio ya mitahini katika Taifa Leo ni daraja halisi la mafanikio kwa wengi wa wanafunzi wanaotumia maswali hayo mara kwa mara kujipiga msasa na kujitia kwenye mizani.

Chama huandaa vikao vya mara kwa mara kwa lengo la kuwashirikisha wanafunzi kikamilifu katika mashindano yanayolenga kubaini upekee wa vipaji vyao katika utangazaji wa habari na utunzi wa kazi bunilizi.

Kuwepo kwa chama hiki shuleni Kitengela International Syokimau kumeamsha ari ya mapenzi ya Kiswahili miongoni mwa wanachama ambao kwa sasa ni mabalozi halisi wa Kiswahili na wasomaji wakubwa wa gazeti hili la Taifa Leo.

You can share this post!

Wafungwa waachiliwa kupunguza msongamano

PSG tayari kumsajili Ronaldo kucheza na Messi