• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
OKA WAKAA NGUMU!

OKA WAKAA NGUMU!

Na LEONARD ONYANGO

VIONGOZI wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA) wamesisitiza kuwa wataunga mmoja wao kuwania urais 2022 huku vyama vya ODM na Jubilee jana vikitangaza rasmi kuungana.

Kwenye mkutano wa siku mbili uliofanyika katika Hoteli ya Great Rift Valley, Naivasha, kaunti ya Nakuru, viongozi wa OKA – Kalonzo Musyoka (Wiper), Gideon Moi (Kanu) na Musalia Mudavadi (ANC) – hata hivyo, walikosa kutaja ni nani miongoni mwao atawania urais.

“Tumekubaliana kwa kauli moja kwamba, muungano wa OKA utakuwa na mwaniaji wa urais 2022. Mwaniaji atakayepeperusha bendera ya OKA yuko hapa,” wakasema viongozi wa OKA.

Viongozi hao walisema kwamba, wamefurahishwa na hatua ambazo wamepiga katika kusuka muungano wao na kusisitiza kuwa wataungana hadi kwenye debe.

Iwapo watashikilia msimamo huu, huenda juhudi za Rais Uhuru Kenyatta za kuwataka wamuunge kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga zikagonga mwamba.

Rais Kenyatta alikutanisha viongozi wa OKA na Bw Odinga katika ikulu ya Mombasa na kuwataka washirikiane kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Kilomita chache kutoka katika hoteli ya Great Rift Valleywalikokutana, kulikuwa na mkutano ulioongozwa na Bw Odinga mjini Nakuru ambapo vyama vya ODM na Jubilee vilitangaza rasmi kuungana.

Bw Odinga alizindua vuguvugu la Azimio la Umoja ambalo analenga kulitumia kupenya katika eneo la Mlima Kenya akihubiri amani, utangamano, upendo, msamaha na ufufuaji wa uchumi.

Uzinduzi huo ulifanyika saa chache baada ya Kamati ya Usimamizi ya Jubilee (NMC) kukutana jijini Nairobi na kuidhinisha sekretariati ya chama hicho tawala kuanzisha mchakato wa kuungana na ODM.

Kamati ya NMC iliagiza sektretariati ya Jubilee kuandikia barua vyama vya Wiper na Kanu kuvifahamisha kuhusu uamuzi wa kutaka kuungana na ODM.

Chama cha Kanu kilitia mkataba wa kuungana na Jubilee kabla ya uchaguzi wa 2017. Chama cha Kanu kimekataa kutia saini mkataba wa kujiunga rasmi na OKA huku kikisema kuwa kingali mshirika wa Jubilee na hakiwezi kuwa kwenye miungano miwili.

Chama cha Wiper kilitia saini mkataba wa kushirikiana na Jubilee mnamo Juni 2020.Baada ya Wiper kujiondoa kutoka muungano wa NASA, mwezi uliopita, Bw Musyoka alitangaza kuwa chama hicho kitaendelea kushirikiana na Jubilee.

“Chama cha Jubilee kitaandika barua rasmi kufahamisha Kanu na Wiper kuhusu uamuzi wa kuungana na ODM. Mlango wa kufanya mazungumzo na washirika wetu (Kanu na Wiper) uko wazi,” akasema Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju.

Jana, Bw Odinga aliwataka Wakenya wote kuungana kuinua uchumi na kudumisha amani nchini.“Hatuna budi kuungana ili tuinue uchumi wetu.

Tusikubali wanasiasa kutumia umaskini na ukosefu wa ajira nchini kama chombo cha kujitafutia umaarufu wa kisiasa. Tusikubali wanasiasa kuzua mgawanyiko baina ya matajiri na maskini au kati ya kabila moja na jingine.

“Tunapoelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022, tunafaa kutakasa nchi yetu na kuondoa roho mchafu wa chuki na hasira ili tujenge nchi yetu pamoja,” akasema Bw Odinga.

Viongozi kutoka eneo la Mlima Kenya waliohudhuria hafla ya Nakuru, walimiminia sifa Bw Odinga huku wakimtaja kama kiongozi mwenye busara, tajiriba na uwezo wa kuongoza Kenya baada ya uchaguzi ujao.

“Sisi watu wa Mlima Kenya hatujazoea upinzani na hatuko tayari kwenda upinzani kwa kuunga mkono watu wengine,” akasema Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru huku akirejelea Naibu wa Rais William Ruto.

Bi Waiguru alisema kuwa baada ya mkutano wa jana, Bw Odinga ataanza kuzuru maeneo mbalimbali ya Mlima Kenya ili kusaka kura.

“Raila akitangaza tu kuwania urais tayari amepata asilimia 40 ya kura kabla ya hata kutangaza mwaniaji mwenza. Akitangaza mwaniaji mwenza wake anapata zaidi ya asilimia 50 ya kura. Kwa hiyo watu watu wa Mlima Kenya wakidanganywe na yule (DkR Ruto) watajipata nje ya serikali,” akasema Bi Waiguru.

Naye mbunge wa zamani wa Gatanga Peter Kenneth alisema kuwa viongozi wanaounga mkono handisheki watamtembeza Bw Odinga katika eneo la Mlima Kenya ili akutane na wakazi.

You can share this post!

Rais aongoza Wakenya kuomboleza seneta aliyefariki kwa ajali

Viongozi wa kutoka Mlima Kenya wakutana Thika kuweka...