• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
CECIL ODONGO: Kuna dalili uchaguzi wa 2022 huenda urudiwe

CECIL ODONGO: Kuna dalili uchaguzi wa 2022 huenda urudiwe

Na CECIL ODONGO

HUENDA ikawa vigumu kuepuka duru ya pili katika uchaguzi mkuu wa 2022 huenda ikawa vigumu kuepukika, ikizingatiwa kuwa ni vigumu kwa wawaniaji ambao wametangaza azma yao ya kuingia ikulu, kujihakikishia uungwaji mkono wa zaidi ya asilimia 50 jinsi inavyoamrisha Katiba.

Inaonekana wanasiasa wakuu wanaomezea mate kiti cha urais wametambua hilo, ndiposa kuna juhudi za kubuni miungano mipya ya kisiasa.Ingawa ni dhahiri kwamba Naibu Rais William Ruto yupo kifua mbele dhidi ya wawaniaji wengine, atakuwa na kibarua kupata zaidi ya nusu ya kura zote ili kutwaa uongozi.

Tayari uungwaji mkono aliokuwa ameonekana kuvutia katika ukanda wa Mlima Kenya umeanza kutikiswa, baada ya baadhi ya wanasiasa waliokuwa nyuma yake mwanzoni kunywea wakisisitizia umoja wa eneo hilo.

Kiongozi wa The Service Party (TSP) Mwangi Kiunjuri, na mwenzake wa Chama Cha Kazi Moses Kuria, ambao wamekuwa wandani wa Dkt Ruto wameanza kusitasita wakisema vyama hivyo havitavunjwa ili waingie ndani ya UDA ya Naibu Rais.

Mwanasiasa mkongwe Martha Karua, ambaye pia ni mwenyekiti wa Narc-Kenya, naye alisisitiza kwamba eneo hilo bado halijaafikia kuhusu mgombea watakayemuunga 2022.

Nafasi ya Dkt Ruto kuvuna kura zote za mlimani inadidimizwa zaidi na mivutano kati ya mirengo ya Kieleweke na Tangatanga.

Pamoja na tangazo la Spika wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi, kwamba atakuwa debeni mwaka ujao Bw Muturi ameonekana kuungwa mkono na wanasiasa wa Mlima Kenya Mashariki ambao wanawalaumu wenzao kutoka Mlima Kenya Magharibi kwa kuwasaliti licha ya kuunga mkono tawala za Mzee Jomo Kenyatta, Mwai Kibaki na Rais Uhuru Kenyatta.Isitoshe Kinara wa ODM Raila Odinga ameanza kupenya mlimani kando na kuweka mikakati ya kujiongezea umaarufu kupitia kampeni kabambe.

Bw Odinga anaaminika kuungwa mkono na mabwenyenye wa eneo hilo pamoja na familia ya Rais Uhuru Kenyatta.Iwapo Dkt Ruto hatapata zaidi ya asilimia 90 za kura za Mlima basi itakuwa kibarua kigumu kufikisha asilimia inayohitajika ya kikatiba.

Hali ni hiyo hiyo kwa kinara wa ODM Raila Odinga ambaye amepoteza baadhi ya wandani wake kwa muungano mpya wa OKA.Rais Kenyatta ameonekana kutambua hili ndiyo maana kumekuwa na juhudi za kuwaleta wanasiasa hao pamoja kuelekea 2022.

Iwapo Kalonzo Musyoka wa Wiper na Musalia Mudavadi wa ANC watawania urais basi Bw Odinga akapoteza uungwaji mkono muhimu Ukambani na Magharibi mwa nchi.Hali wanayojipata ODM na OKA ni kama ile ya kuelekea uchaguzi wa 1992 ambapo upinzani uliungana chini ya Ford ukilenga kukiondoa chama cha Kanu mamlakani.

Mpasuko wa kung’ang’ania uongozi uliotokea baada ya wanasiasa hao kukosa kuaminiana ulimwezesha Rais Daniel Arap Moi kushinda kura hiyo.

Mwanasiasa kama Martin Shikuku ambaye alikuwa mrengo wa Oginga Odinga wa Ford Kenya ni kati ya walioshangaza kwa kuvuka dakika za mwisho upande wa Ford Asili uliokuwa ukiongozwa Kenneth Matiba.

Vivyo hivyo, kuna uwezekano baadhi ya viongozi wa OKA wanaweza kuvukia upande wa Dkt Ruto na kudidimiza zaidi Urais wa Bw Odinga.

Kwa hivyo, itabidi Dkt Ruto na Bw Odinga waweke mbinu na mikakati ili kukumbana na vizingiti ambavyo vitaishia wao kushiriki duru ya pili ya uchaguzi.

You can share this post!

Lewandowski aongoza Bayern kukomoa Dortmund na kutwaa...

LEONARD ONYANGO: Wawaniaji urais walipe uzito suala la...