• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Amerika yafungia Taliban pesa

Amerika yafungia Taliban pesa

Na MASHIRIKA

AMERIKA imefunga akaunti za Benki Kuu ya Afghanistan zenye Sh950 bilioni ili kuuzuia utawala mpya wa Taliban kupata fedha kuiendesha serikali yake.

Kulingana na afisa mmoja wa ngazi za juu wa serikali ya Amerika, taifa hilo pia limesimamisha shughuli za usafirishaji wa fedha nchini Afghanistan.

Afisa huyo vile vile alisema Amerika itashikilia mali yoyote inayomilikiwa na benki hiyo, hivyo kuuzuia utawala wa Taliban kuifikia kwa namna yoyote ile.

Taliban ni miongoni mwa makundi ambayo yamewekewa vikwazo vya kifedha na Amerika. Makundi mengine ni Hizbollah, Al-Qaeda, Hamas, Boko Haram kati ya mengine.

Kaimu Afisa Mkuu wa benki hiyo, Ajmal Ahmady, alisema alifahamu mapema wiki hii kwamba Amerika imesimamisha shughuli zozote za kusafirisha fedha nchini humo.

Fedha hizo zinatajwa kuwa muhimu katika kuiwezesha Taliban kuendeleza utawala wake ikiwa ingefaulu kuzipata.Vikwazo hivyo vinamaanisha huenda utawala wa Taliban usifanikiwe kuzifikia fedha hizo kwa vyovyote vile.

Sehemu kubwa ya mali inayomilikiwa na benki haipo Afghanistan, kulingana na maafisa wakuu wanaosimamia shughuli zake.Wizara ya Fedha ya Amerika ilikataa kutoa taarifa yoyote kuhusiana na hatua hiyo.

Hatua hiyo inajiri huku kamanda mkuu wa kundi la Haqqani Network, Annas Haqqani, akikutana na aliyekuwa rais wa taifa hilo, Hamid Karzai, kwa mazungumzo maalum.

Kundi hilo lina uhusiano wa karibu na Taliban.Duru zilisema mazungumzo hayo yaliangazia juhudi za wapiganaji hao kubuni serikali.

Karzai alikuwa ameandamana na mjumbe mkuu wa amani katika uliokuwa utawala wake, Abdullah Abdullah.

Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusu kikao hicho.Kundi la Haqqani limekuwa likilaumiwa kwa kuwasaidia wapiganaji wa Taliban kutekeleza mashambulizi kwenye mpaka wa Afghanistan na Pakistan kwa miaka mingi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, amesema utawala wa Taliban utaaminiwa kwa vitendo vyake wala si ahadi unazotoa.Wanamgambo hao wamesema wanataka amani, na hawatalipiza kisasi dhidi ya maadui wao wa jadi.

Wamesema pia wataheshimu haki za wanawake, japo kwa misingi ya sheria na kanuni za dini ya Kiislamu.Hata hivyo, maelfu ya raia wa taifa hilo wanahofia kuwa huenda wapiganaji hao wakakosa kutimiza ahadi zao. Wengi wao tayari wameanza kuondoka na kutorokea nchi jirani.

“Tutauamini utawala huu kulingana na vitendo na sera itakazoanza kutekeleza. Tutafuatilia jinsi utakavyoshughulikia masuala muhimu kama ugaidi, ulanguzi wa mihadarati, hali ya kibinadamu na haki za wanawake kupata elimu,” akasema Johnson, kwenye hotuba maalum aliyotoa kwa Bunge.

Nchi mbalimbali duniani zimetoa ahadi za kuwapa hifadhi raia wa taifa hilo wanaotoroka kwa hofu ya kudhulumiwa na utawala huo.

You can share this post!

Vijana wataka vyuo vya kiufundi vianzishe masomo ya...

Raila sasa tayari kukubali reggae ikizimwa kabisa