• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Dalili Kingi atafuta makao mapya OKA

Dalili Kingi atafuta makao mapya OKA

ANTHONY KITIMO na ALEX KALAMA

GAVANA wa Kilifi, Bw Amason Kingi, ameanzisha mashauriano na Muungano wa One Kenya Alliance.

Gavana huyo Alhamisi alikutana na vinara wa OKA katika hoteli iliyo Mombasa, na kuashiria uwezekano wake kuwakilisha ukanda wa Pwani ambao kufikia sasa, umeonekana kukosa uwakilishi katika mashauriano ya kuunda miungano ya kisiasa.

Hatua hiyo ya Bw Kingi imetokea siku chache baada ya Chama cha ODM kumpokonya wadhifa wake wa uenyekiti katika Kaunti ya Kilifi, huku viongozi wa vyama vitano alivyotaka viungane ili viunde muungano mmoja wa Pwani wakijitenga naye.

Jana, alikutana na Kiongozi wa Chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, mwenzake wa Wiper, Kalonzo Musyoka, na Seneta wa Bungoma, Moses Wetang’ula, ambaye ni Kiongozi wa Ford-Kenya.

Bw Musyoka aliashiria kulikuwa na sababu ya Bw Kingi kuwepo mahali ambapo walikuwa wanakutana, ingawa alikataa kutoa maelezo zaidi.

“Ukiona vyaelea jua vyaundwa,” Bw Musyoka akaambia wanahabari.Bw Kingi, ambaye duru zimesema wandani wake wanaendeleza mipango ya kuzindua rasmi chama kipya, alithibitisha kufanya kikao na watatu hao.

“Niliwakuta baadhi ya vinara wa OKA Mombasa tukazungumza kwa muda mfupi na kukubaliana kwamba kunahitajika kuwe na mazungumzo rasmi,” akasema Bw Kingi.

Kaimu Mwenyekiti wa ODM tawi la Kaunti ya Kilifi, Bw Teddy Mwambire alisema chama hicho hakijapokea barua rasmi kutoka kwa viongozi ambao wanadai kukihama, kwa hivyo haifai kusemekana wamehama.

Kando na Bw Kingi, wengine walioasi ODM Kilifi ni Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, na mwenzake wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya.

“Usistaajabu ukisikia kwamba wamerudi kwa sababu bado hawajaandika barua ya kuonyesha wamehama kwa chama. Mtu hawezi kuhama halafu awe amebakia. Gavana Kingi bado ni mwenyekiti wetu katika tawi la Magarini na bado ni mwanakamati mkuu katika kikosi cha kaunti nzima ambacho mimi nitakuwa ndiye mwenyekiti,” alisema Bw Mwambire akiwa katika eneo la Karimani, Kilifi.

Vinara hao wa OKA walikuwa wamekutana na Rais Uhuru Kenyatta pamoja na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, na Seneta wa Baringo, Bw Gideon Moi ambaye ni Mwenyekiti wa KANU mnamo Jumatatu katika ikulu ya Mombasa.

Duru zilikuwa zimeambia Taifa Leo kwamba, mkutano huo wa Jumatatu ulikuwa ni juhudi zaidi za rais kuwashawishi wawe ndani ya muungano mmoja na kusimamisha mwaniaji mmoja wa urais katika uchaguzi ujao, lakini jana walisisitiza walishauriana tu kuhusu kanuni za kudhibiti ueneaji wa virusi vya corona.

Rais Kenyatta na wandani wake wanataka Bw Odinga aungwe mkono katika muungano utakaoundwa, lakini kila kinara anashikilia kuwa ndiye ametosha kuwania urais 2022.

“Hakuna mtu aliomba wala hata kupendekeza kwamba tumuunge mkono mtu yeyote kwa wadhifa wowote,” akasema Bw Mudavadi.

Naibu Kiongozi wa ANC, Bw Ayub Savula alisema kambi ya OKA ilikuwa ikimtafuta Bw Kingi kwa muda mrefu.

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Darubini kwa Chebukati uchaguzi wa 2022...

KDF kusaka sare zilizo mikononi mwa raia