• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Wauguzi wagomea chanjo ya corona licha ya amri kali

Wauguzi wagomea chanjo ya corona licha ya amri kali

Na Shaban Makokha

WAUGUZI katika Kaunti ya Kakamega hawaonekani kuchangamkia chanjo ya corona licha ya Wizara ya Afya kusema ni lazima kwa wahudumu wote wa afya nchini.

Imebainika wengi wao wamesita kupokea chanjo hiyo huku wakionekana kutoshughulika licha ya kutangamana na kuwatibu wanaougua corona.

Afisa wa Afya anayehusika na kuwapandisha wauguzi vyeo Tabitha Kiberenge alisema kuwa ni wauguzi wachache tu waliojitokeza licha ya kuwa jukumu lao linawaweka katika hatari ya kuambukizwa virusi hivyo.

Bi Kiberenge alitoa wito kwa wauguzi hao wajizatiti na kupokea chanjo ya corona ili kuwa kielelezo bora kwa raia ambao pia wamekosa kuchangamkia chanjo yenyewe.

Bila kutoa takwimu maalum, Bi Kiberenge alisema kuwa idadi ya wauguzi waliopokea chanjo ya corona ni wachache mno na hata haifikii nusu ya wote walioajiriwa katika kaunti hiyo.

“Wauguzi kwa kuwa walioko mstari wa mbele katika kutoa huduma za kiafya wanafaa kuheshimu amri hii. Wanafaa wapokee chanjo na kuondoa dhana na ukosefu wa imani katika chanjo inayotolewa miongoni mwa raia,” Bi Kiberenge.

Waziri wa Afya wa Kakamega Dkt Collins Matemba aliwaonya wauguzi hao dhidi kuwa wasihatarishe maisha yao kwa kukataa chanjo ilhali wenzao kote ulimwenguni wananufaika na chanjo hiyo.

You can share this post!

KDF kusaka sare zilizo mikononi mwa raia

Binti adai kupigwa sababu hajakeketwa