• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 4:28 PM
Hatujaunga mkono Raila wala Ruto – Viongozi Mlima Kenya

Hatujaunga mkono Raila wala Ruto – Viongozi Mlima Kenya

Na JAMES MURIMI

BAADHI ya viongozi wa Jubilee kutoka eneo la Mlima Kenya wamekanusha kuwa wanaunga mkono azma ya urais wa kinara wa ODM Raila Odinga au mwaniaji yeyote yule kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Viongozi hao wakiwemo magavana Anne Waiguru (Kirinyaga), James Nyoro (Kiambu) na Ndiritu Mureithi (Laikipia) pamoja na wabunge Amos Kimunya (Kipipiri), Kanini Kega (Kieni), Jeremiah Kioni (Ndaragwa) na Sabina Chege (Murang’a) waliandaa mkutano katika hoteli ya Kambi Msituni, Laikipia Magharibi ambako walisema kuwa eneo hilo bado halijitangaza kuwa “liko nyuma ya Bw Odinga au mwaniaji yeyote wa urais”.

Bi Waiguru alikanusha kuwa Rais Uhuru Kenyatta amewaelekeza ‘kumuuza’ Bw Odinga katika eneo hilo lenye wapigakura wapatao milioni tano.

“Hatujawa tukimuuza Bw Odinga kwa wapigakura wa eneo hili. Tunawakaribisha wawaniaji wote wa urais wasake kura Mlima Kenya mradi watuahidi kuwa watazingatia maslahi yetu,” akasema Bi Waiguru.

Kauli yake iliungwa mkono na Bi Chege ambaye alisisitiza kuwa watamuunga mkono mwaniaji wa urais mwenye nia ya kuinua uchumi wa Mlima Kenya akiingia mamlakani.

“Bado hatujaamua kuwa tutamuunga mkono mwaniaji fulani wa urais. Lazima maslahi yetu yajumuishwe kwenye manifesto ya kiongozi tutakayetangaza kumuunga mkono,” akasema mwakilishi huyo wa kike wa Kaunti ya Murang’a.

Viongozi hao pia walikariri kuwa wanaheshimu uamuzi wa mahakama ya rufaa ulioangusha kabisa mchakato wa marekebisho ya katiba kupitia BBI uliokuwa ukisukumwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga.

“Tunaheshimu uamuzi ambao ulitolewa na jopo la majaji saba. Tunashauriana na mawakili wetu wa kikatiba ili kupata mwelekeo kuhusu suala hilo. Tumekuwa na mpango fiche hata kabla ya uamuzi wa mahakama na hatutafichua hayo kwa sasa,” akasema Bw Kioni.

Mbw Nyoro na Mureithi walisema kuwa walijadiliana kuhusu namna ya kukwamua uchumi wa eneo hilo ambao umeathirika sana kutokana na baadhi ya sera hasi za kiuchumi za serikali kuu.

“Tumejadiliana kuhusu namna ya kuwasaidia wafanyabiashara wetu ambao wamekuwa wakiteseka hasa wale wanaoagiza bidhaa nje ya nchi. Kutokana na masharti makali yaliyowekwa na serikali, biashara za watu wetu ndizo zimeathirika zaidi,” akasema Bw Nyoro.

You can share this post!

Hofu Ulaya ikipunguza chanjo za Covid-19 Afrika

BBI: Ruto asifu mahakama na kumshauri Uhuru