• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
BBI: Ruto asifu mahakama na kumshauri Uhuru

BBI: Ruto asifu mahakama na kumshauri Uhuru

Na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto jana alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kurejelea miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na Jubilee, baada ya Mpango wa Kubadilisha Katiba (BBI) kutupwa na Mahakama ya Rufaa mnamo Ijumaa.

Akiwahutubia wanahabari katika makazi yake, mtaani Karen, jijini Nairobi jana, Dkt Ruto alisema wakati umefika kwa Rais kuelekeza upya juhudi zake katika Ajenda Nne Kuu za Maendeleo ili kuwafaidi Wakenya.

“Ninaamini bado kuna muda wa kurejelea ajenda tulizoanzisha kuwafaidi Wakenya baada ya kupoteza muda na fedha nyingi kwa masuala mengine,” akasema.

Alisifia uamuzi wa majaji wa mahakama hiyo, akisema umedhihirisha Katiba ya nchi inaendelea kujitetea.Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi Kenya (COTU) amesema kuwa Mpango wa Kubadilisha Katiba (BBI) utafufuliwa tena baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Kwenye taarifa jana, Bw Atwoli alisema licha ya uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kufutilia mbali mchakato huo, bado kuna tatizo kuhusu mfumo wa utawala nchini.

Bw Atwoli alisema mfumo wa sasa wa utawala ndio umekuwa chanzo cha ghasia na machafuko ya kisiasa ambayo yamekuwa yakiikumba nchi kila baada ya miaka mitano uchaguzi unapokaribia.

“Ningetaka kuwaambia Wakenya kuwa jambo la kwanza kwa serikali itakayochukua uongozi mnamo 2022 ni kuibadilisha Katiba. Hii ni kutokana na hali ya taharuki itakayokuwa nchini,” akasema Bw Atwoli.

Katibu huyo ni miongoni mwa viongozi ambao wamekuwa katika mstari wa mbele kuupigia debe mpango huo.Viongozi wengine waliotoa kauli zao ni kiongozi wa ODM, Raila Odinga, Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper) kati ya wengine.

Bw Odinga alisema uamuzi huo si mwisho, bali ni sehemu ya mazungumzo ambayo Wakenya wataendelea kuwa nayo katika siku zijazo.

You can share this post!

Hatujaunga mkono Raila wala Ruto – Viongozi Mlima...

BBI: Uhuru, Raila sasa kusuka mbinu mpya ya mageuzi