• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
Madiwani waasi ODM baada ya Kingi kuadhibiwa

Madiwani waasi ODM baada ya Kingi kuadhibiwa

Na MAUREEN ONGALA

CHAMA cha ODM kimepata pigo tena katika Kaunti ya Kilifi, baada ya baadhi ya madiwani kukataa wito wa Kaimu Mwenyekiti, Bw Teddy Mwambire, kuungana kwa maandalizi ya uchaguzi ujao.

Bw Mwambire ambaye pia ni Mbunge wa Ganze, alikuwa ameandaa mkutano na wanachama wa ODM eneo hilo wikendi, ambapo walitarajiwa kujadiliana kuhusu jinsi watakavyokabiliana na wimbi la uasi dhidi ya chama hicho lililotanda katika kaunti hiyo.

Baadhi ya madiwani waliohudhuria mkutano huo, wakiongozwa na Naibu Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kaunti, Bw Sammy Ndago, walikataa wito wa kuendelea kuwa waaminifu chamani.

Badala yake, walisema wataungana na Gavana Amason Kingi, ambaye hivi majuzi alipokonywa wadhifa wake wa uenyekiti katika ODM kwa sababu ya msimamo wake mkali wa kupania kuunda chama cha Pwani.

Msimamo huo wake ulikuwa umepingwa na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, ambaye alishikilia kwamba utasababisha siasa za kikabila.

“Sisi bado tunampenda Baba (Bw Odinga) lakini tuna njia zetu tunazotaka kufuata Pwani. Hii si siri, na tutawapa wafuasi wetu mwelekeo wa kisiasa ifikapo Septemba. Wapwani wamechoshwa na jinsi wanavyonyimwa haki katika uongozi wa kisiasa kitaifa,” akasema Bw Ndago.

Kulingana naye, wanasiasa wengi waliounga mkono ODM Kilifi walifanya hivyo kwa kufuata ushauri wa Bw Kingi na sasa hawako tayari kujitenga naye.

Msimamo wake uliungwa mkono na Diwani wa Sokoni, Bw Gilbert Peru ambaye alisema chama kipya kinachohusishwa na Bw Kingi kitakomboa Pwani kisiasa.

Alifichua kuwa chama hicho cha Pamoja Alliance (PAA) kitaingia katika miungano ambayo itajitolea kufanikisha haki kwa Wapwani.

Hivi majuzi, Bw Kingi alidokeza uwezekano wake wa kujiunga na Muungano wa One Kenya Alliance (OKA).

Diwani wa Kibarani, Bw John Mwamusti, alisema chama hicho ndicho kitakachowakilisha maslahi ya eneo la Pwani kwa serikali kuu.

“Kila eneo lina chama chake ambacho kinatambulika kitaifa. Itakuwa vyema kama Pwani itafuata jinsi wengine wanavyofanya. Tutakuwa wajinga kama hatutajipanga kabla ya uchaguzi ujao,” akasema Bw Mwamusti.

Mbali na wanaotaka kujiunga na chama cha Pwani ambacho kinasubiriwa kuzinduliwa, wanachama wengine wakiongozwa na Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa waliamua kuungana na Naibu Rais, Dkt William Ruto.

Hata hivyo, wanachama ambao bado ni waaminifu kwa ODM walisisitiza kuwa hawatatishwa na matukio yanayoashiria kuwa chama hicho kimepoteza ufuasi Kilifi.

Bw Mwambire alitoa changamoto kwa wale ambao hawataki kuendelea kuwa wanachama wahame ili kuwapa wanachama halisi nafasi ya kujiandaa kwa uchaguzi ujao.

Kulingana naye, matukio yanayoshuhudiwa sasa yaliwahi kushuhudiwa awali lakini ODM bado ikaendelea kuwa maarufu.

“Kila mtu anafahamu matukio ya kabla uchaguzi wa 2013. Baadhi ya madiwani na wabunge waliokuwa ODM walitoroka chama, lakini ODM ikavuna viti vingi 2017. Tulipata viti vyote vya ubunge,” akasema.

Alisema kuwa katika miezi mitatu ijayo, chama hicho kitakuwa na muundo mpya ikiwemo kuwa na viongozi wapya na afisi katika maeneobunge yote saba na wadi 35.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Seneta wa Kilifi, Bw Stewart Madzayo, na Mbunge wa Kilifi Kusini, Bw Ken Chonga na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kaunti, Bw Mwathethe Kadenge.

You can share this post!

ODONGO: Kifo cha BBI chaweka OKA hatarini zaidi 2022

Uhuru, Raila wahudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais...