• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:16 PM
KAMAU: Masaibu ya Wakenya Arabuni yakome sasa

KAMAU: Masaibu ya Wakenya Arabuni yakome sasa

Na WANDERI KAMAU

SIMULIZI za Wakenya wanaokumbana na mateso katika nchi za Arabuni ni za kuatua moyo.

Binafsi, nimechoshwa na simulizi hizi za kuogofya.

Naam, nimechoka kuwasikia akina dada wetu wakieleza madhila, mahangaiko na hujuma wanazokumbana nazo katika nchi za Ghuba.

Nimeacha hata kutazama video wanazotuma kutoka katika nchi hizo, kwani huwa najikuta nikibubujikwa na machozi.

Mara nyingine, huwa nashindwa hata kufanya kazi zangu binafsi ninapowaza kuhusu hali wanazojikuta akina dada hao.Hata hivyo, hali hii imedumu kwa muda mrefu.

Ni miaka na mikaka sasa tangu nilipoanza kusikia malalamishi ya wanawake wanaoenda kufanya kazi katika mataifa hayo.

Swali langu ni: Hali hii itatatuliwa vipi? Wahusika wakuu wako wapi? Huwa wanachukua hatua zozote? Huwa wanatazama au kufikiwa na vilio hivyo?

Ni taswira za kusikitisha wakati familia zinaagana na jamaa zao wakiwa hai wanapoelekea huko na baadaye kurejea wakiwa maiti.

Kulingana na tamaduni za Kiafrika, si vizuri wakati mzazi anapomzika mwanawe.

Hata hivyo, hali ndivyo imekuwa kwa vijana barobaro wanaoenda Arabuni, kwani baadhi yao wamerejeshwa makwao wakiwa kwenye majeneza—wasijue wala kufahamu yanayoendelea.

Sikitiko jingine ni kuwa familia nyingi huwa zinafahamishwa kuhusu vifo vya jamaa zao wiki kadhaa au hata baada ya miezi tangu wakati wanapofariki.

Pengine hakuna huzuni kubwa kuliko kama hiyo katika maisha tuishiyo hapa duniani.Katika mvurugiko huu wote wa matukio, ni nani anapaswa kulaumiwa?

Mnamo 2016, serikali ilipiga marufuku kwa muda usafirishaji wa wafanyakazi kutoka Kenya kuelekea katika mataifa hayo, hadi pale mchakato wa kubuniwa kwa taratibu za kudhibiti mazingira yao ya kufanyia kazi ungekamilika.

Baada ya karibu miaka minne, serikali ya Kenya, Saudi Arabia na mataifa mengine kadhaa zilitangaza kufikia mkataba kuhusu haki za wafanyakazi hao ambazo lazima zizingatiwe na waajiri wao pale wanapoanza kuwafanyia kazi.

Mkataba huo pia ulijumuisha taratibu ambazo lazima zizingatiwe na mashirika yanayowasafirisha wafanyakazi katika mataifa hayo.

Pendekezo jingine lililojumuishwa kwenye maafikiano hayo ni kuwa lazima mashirika hayo yawe yamesajiliwa rasmi, ili kuhakikisha yanaendesha shughuli zao kwa misingi na taratibu za kisheria zilizowekwa.

Hata hivyo, maafikiano hayo yalionekana kuwa tiba ya muda tu, kwani simulizi zimekuwa ni zile zile.

Vilio na majonzi yasiyoisha.

Tulikofikia, ni wakati serikali ilainishe na kudhibiti hali hii.Familia zinazoathiriwa zimekuwa zikiulaumu ubalozi wa Kenya nchini Saudi Arabia kwamba huwa hautilii maanani malalamishi yanayowasilishwa kwake.

Katika kujitetea kwake, ubalozi hao umekuwa ukiwalaumu Wakenya wanaoathiriwa kwa kutumia njia za mkato kuingia katika nchi hizo kutafuta ajira.

Bila shaka, lawama hizi hazitatusaidia hata kidogo kaka jamii.Badala yake, tutaendelea kulaumiana huku familia zikiendelea kuwapoteza wapendwa wao mikononi mwa watu wasiojali wala kuthamini maisha ya mwanadamu.

Suala hili linapaswa kuangaliwa upya kwa kuwajumuisha wadau wote, ikiwemo Wizara ya Mashauri ya Kigeni.

Lazima mwafaka huo utathminiwe tena ili kuhakikisha makubaliano yote yaliyofikiwa yanazingatiwa na kila mmoja. Kwa hilo, huenda taswira tunazoshuhudia zikafikia kikomo.

[email protected]

You can share this post!

ARTETA: Ana wiki sita tu!

KINYUA BIN KING’ORI: Hongera Uhuru na Raila kukubali...