• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Vita vya kujipima nguvu ugavana Kiambu vyaanza

Vita vya kujipima nguvu ugavana Kiambu vyaanza

Na LAWRENCE ONGARO

KITI cha ugavana Kaunti ya Kiambu kimeongeza joto la kisiasa huku viongozi kadhaa wakianza kuelezea nia zao.

Tayari Gavana wa Kiambu, Dkt James Nyoro na mbunge wa Thika Bw Patrick Wainaina, wamejitosa ulingoni na kutangazia wafuasi wao kuwa wako tayari kuwania kiti hicho.

Mnamo Jumatano akiwa mjini Thika, Dkt Nyoro alisema kwa zaidi ya mwaka mmoja ametekeleza mambo mengi yanayoweza kutambulika na wananchi.

Akihutubia wakazi wa mtaa wa Kisii mjini Thika, gavana huyo alisema maendeleo aliyofanya yanaonekana na kwa hivyo wananchi hawastahili kuelezwa isipokuwa wao kujionea wenyewe.

“Mimi sitaki kujitangaza kwa wananchi lakini kila mmoja akitembea kaunti ya Kiambu atajiamulia na kujionea mwenyewe yaliyofanywa kimaendeleo,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema barabara katika kaunti ndogo 12 zilizoko Kiambu zimefanyiwa ukarabati ambapo hali ya usafiri ni rahisi kwa kila mkazi wa huko na wahudumu wa usafiri.

Wakati huo pia alisema umeme na maji yamesambazwa kila sehemu na kwa hivyo kila mkazi wa Kiambu anajionea vitendo.

Matamshi yake yalikubaliwa na diwani Bi Emma Wanjiku ambaye alisema wananchi wanastahili kuwa makini wakati wanapofanya uamuzi wa viongozi wanaowataka.

“Wakati huu sio wakati wa kupiga siasa lakini ni wa kazi. Ikifika mwaka ujao kila mmoja atajitambulisha na kueleza aliyofanya,” alisema Bi Wanjiku.

Aliwashauri wasitekwe nyara na propaganda bali wawe makini na kutathmini yote yaliyofanywa na viongozi wao.

Naye Bw Wainaina ambaye ni mbunge wa Thika, alisema kila kiongozi ni sharti aje na ajenda maalum ya kusaidia vijana.

Alisema ajenda yake kuu akipata nafasi ya kuwa gavana ni kuwahamasisha vijana.

“Tunaelewa ya kwamba asilimia kubwa ya vijana hawana ajira, na kwa hivyo ni bora kutafuta mbinu ya kuwasaidia,” alifafanua mbunge huyo.

Alisema asilimia 80 ya vijana ni wale hawana ajira na itakuwa vyema kupunguza kiwango hicho ili kishuke hadi asilimia 20.

Alisema kwa miaka minne amekuwa uongozini akiwa mbunge amekarabati shule za msingi zipatazo 30 na kuzigeuza kuwa bora zaidi.

Alisema hata wanafunzi wa shule hizo wanajisikia wakiwa katika mazingira mapya pamoja na walimu wao.

Alisema kitu cha muhimu ni kuleta vijana pamoja na kuwahimiza wabuni ajira baada ya kuwapa mikopo.

Alieleza kuwa kuna mbinu nyingi za kubuni kazi na hiyo ndiyo njia pekee ya kuwapa vijana nafasi ya kujitegemea kimaisha.

Alitaja Kiambu kama eneo ambalo lina wafanyabiashara wengi huku akisema vijana wengi watanufaika wakipewa mwongozo unaofaa wa kufanya biashara.

Alisema iwapo kaunti zitaongezwa kuwa na fedha zaidi za maendeleo, bila shaka kutakuwa na mageuzi mengi ya kimaendeleo.

You can share this post!

Cristiano Ronaldo arejea Manchester United baada ya kuagana...

Leicester City kupimana ubabe na Napoli katika Europa League