• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
TSC yapata ngao kuzuia walimu kujihusisha na ubodaboda

TSC yapata ngao kuzuia walimu kujihusisha na ubodaboda

Na FAITH NYAMAI

VISA vya walimu kuchelewa kufika shuleni wakijihusisha na shughuli zao za kibinafsi kama vile kuendesha bodaboda, vimepungua.

Ripoti ya Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) inasema kuwa tangu kuanzisha kwa Mfumo wa Kielektroniki wa Kuripoti Utendakazi wa Walimu (TPAD), idadi kubwa ya walimu wamekuwa wakifika mapema shuleni na visa vya utoro vimepungua kwa kiasi kikubwa.

Ripoti hiyo iliyotolewa Ijumaa na TSC inasema kuwa visa vya walimu kuzembea kwa kukosa kufundisha wanapokuwa shuleni pia vimeenda chini.

Kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo miaka mitano iliyopita, baadhi ya walimu walishutumiwa kwa kuanza kufanya biashara zao asubuhi kama vile kuendesha bodaboda na kwenda shuleni baadaye mchana.

Wengine walikosa kwenda shuleni kimakusudi huku wanafunzi wakikosa kufundishwa.

“Mfumo wa TPAD umepunguza visa vya kuchelewa na utoro miongoni mwa walimu. Mfumo huo umepunguza visa ambapo walimu walikuwa wakilaza damu shuleni bila kwenda madarasani kufundisha wanafunzi,” inasema ripoti hiyo ya TSC.

Mfumo wa TPAD ulianzishwa mnamo 2016 kwa lengo la kufuatilia utendekazi wa walimu ili kuboresha masomo shuleni.Mfumo huo ni miongoni mwa masuala yaliyozua uhasama baina ya TSC na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu (Knut) Wilson Sossion.

Mnamo 2018, Bw Sossion aliitaka TSC kusitisha matumizi ya mfumo wa TPAD huku akitishia kuitisha mgomo wa walimu kote nchini.

TSC imekuwa ikitumia mfumo huo kufuatilia utendakazi wa zaidi ya walimu 300,000 katika shule za umma za msingi na sekondari katika kaunti zote 47.

You can share this post!

Agizo wanafunzi waliokosa kujiunga na sekondari wasakwe

Hofu msongamano wa chanjo huenda uibue maambukizi