• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Serikali isuluhishe uhaba wa walimu

TAHARIRI: Serikali isuluhishe uhaba wa walimu

KITENGO CHA UHARIRI

JUHUDI za Waziri wa Elimu Prof George Magoha kuhakikisha wanafunzi wa Kidato cha Kwanza wamesajiliwa katika shule za upili hivi majuzi ni za kupongezwa hasa wakati huu ambapo baadhi ya wazazi wamekabwa na ukosefu wa karo kutokana na athari ya janga la corona na njaa.

Waziri Magoha wiki hii alionekana akiwa katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo Pwani na Magharibi kukagua kiwango cha wanafunzi waliopelekwa shuleni za sekondari walikopata nafasi.

Hii ni kuendana na lengo kuu la serikali kuhakikisha kwamba kila mwanafunzi anapata masomo ya sekondari ambayo imeyafadhili. Ili kufikia lengo hili, wazazi wameagizwa wawapeleke watoto wao shuleni huku machifu wakitwikwa jukumu la kuhakikisha amri hiyo imetekelezwa kikamilifu.

Maafisa hawa wanatakikana wawafichue wanaokaidi ili kuchukuliwa hatua faafu kisheria.

Ingawa hatua hii ya serikali ni ya kutia moyo hasa kwa watoto kutoka kwa familia maskini, ripoti kuhusiana na upungufu wa walimu wa baadhi ya masomo ni jambo la kusikitisha na kutaumsha kweli kweli.

Katika mojawapo ya taarifa zetu za toleo la leo, imefichuka kwamba shule 27 nchini zimeathirika kabisa na uhaba wa walimu wa baadhi ya masomo na huenda masomo hayo yakaacha kufunzwa kabisa.

Baadhi ya masomo haya ni ya lazima kama vile Hisabati na Kiswahili. Uhaba huu ulisababishwa na waliosomea ualimu kukosa kutuma maombi ya kazi katika shule hizo husika.

Wengine walituma lakini hawakufika kwa mahojiano hata baada ya kualikwa. Kwingineko, waliohojiwa walikosa kufikia viwango vya kuhitimu vilivyohitajika.

Shule zinazoathirika zinapatikana katika kaunti za Laikipia, Siaya, Nakuru, Kisumu na Kakamega.Ingawa serikali kupitia Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) ilitimiza jukumu lake la kutenga fedha katika bajeti kugharimia uajiri wa walimu 8,914 mwaka huu 2021, ili kukabiliana na uhaba ulioko nchini, tatizo la shule kadhaa kupuuzwa linafaa kuvaliwa njuga na likabiliwe ipasavyo.

Ni wajibu wa wataalamu wa elimu katika wizara kuhakikisha kuna walimu wa kutosha nchini na fauka ya haya kuhakikisha kuna usawa katika uajiri ambapo kila shule itapata walimu wa kutosha bila kujali eneo, kaunti ndogo au kaunti.

Serikali kupitia wizara ya Elimu iibuke na mikakati mahususi kuhakikisha walimu wanapelekwa shuleni ambazo zinakabiliwa na upungufu bila kujali ziko mashambani, vijijini, mashinani au mijini.

Si ajabu kwamba kuna baadhi ya shule ambazo zina walimu wa ziada huku nyingine zikiendelea kuhangaika.

Ni sharti serikali itimizie kila mwanafunzi haki ya kusomeshwa na kupata elimu kwa usawa bila kubagua la sivyo itaonekana kama serikali inayoendeleza maonevu dhidi ya watoto wake.

Hili linawezekana kwani penye nia pana njia. Kazi kwako Profesa Magoha!

You can share this post!

Jinsi ya kuandaa buns zenye ufuta  

DINI: Kuna njaa za aina nyingi ila zipo za lazima...