• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 4:55 PM
Ruto asema kamwe hatajiuzulu

Ruto asema kamwe hatajiuzulu

Na MERCY KOSKEI

NAIBU Rais Dkt William Ruto kwa mara nyingine amekariri kuwa hatajiuzulu kutoka kwa wadhifa wake licha ya kuhangaishwa na serikali anayodai alichangia pakubwa kuingia mamlakani mnamo 2013 na 2017.

Dkt Ruto amesema kuwa wanaomsukuma ajiuluzu wanaota ndoto za Alinacha kwa kuwa kujiondoa katika wadhifa wa naibu rais ni sawa na kuwasaliti Wakenya waliompigia kura pamoja na Rais Uhuru Kenyatta.

Alikuwa akizungumza katika kanisa Katoliki la Mtakatifu Augustine, eneobunge la Bahati, Kaunti ya Nakuru ambapo alikuwa mgeni rasmi.

“Ninawaambia wanaonishauri nijiuzulu kuwa nilipoingia katika siasa, nilifahamu kuwa kuna changamoto tele na suluhu ni kukabiliana nazo badala ya kutoroka. Ninawashukuru kwa ushauri wao ila mimi siendi mahali hadi muhula wangu ukamilike,” akasema Dkt Ruto.

Naibu Rais anaonekana kuendelea kumjibu mkubwa wake Rais Kenyatta ambaye wiki jana akihojiwa na wahariri wa vituo mbalimbali vya habari, alimtaka ajiuzulu iwapo haridhishwi na jinsi ambavyo serikali imekuwa ikiendeshwa.

Badala yake, Dkt Ruto jana aliitaka serikali itafute mbinu ya kutatua shida mbalimbali zinazoathiri mamilioni ya Wakenya ikiwemo kubuni nafasi za ajira kwa vijana badala ya kuendelea kumhangaisha.

“Sikuchaguliwa kuuza aiskrimu ila kusuluhisha matatizo ya Wakenya. Iwapo nitatoroka na kukosa kuyashughulikia matatizo haya, Wakenya watakuwa vipi na imani kuwa nitawasaidia nikichukua usukani?” akauliza.

Aliwataka wanasiasa wasipoteze wakati kwa kuzungumzia kuondolewa kwa maafisa wa GSU waliokuwa wakimpa huduma za ulinzi ambao nafasi zao zilichukuliwa na askari wa utawala (AP).

“Mimi sina tatizo kufanya kazi na maafisa wa AP kwa sababu pengine GSU waliondolewa ili kuwapa Wakenya wengine ulinzi zaidi wanaouhitaji. Hata wakinipa maafisa wa kampuni ya kutoa ulinzi ya G4S bado nitashirikiana nao,” akasema.

Alishikilia kuwa kubadilishwa kwa walinzi wake hakutamzuia kujivumisha miongoni mwa Wakenya kuelekea kura ya 2022.

Seneta wa Nakuru Susan Kihika naye alitaka Idara ya Upelelezi (DCI) iwaamrishe Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli na Katibu katika wizara ya Usalama wa Ndani Karanja Kibicho kufafanua kauli zao kuwa Dkt Ruto hatakuwa kwenye debe mnamo 2022.

“Kisheria walinzi wa Naibu Rais wanafaa wawe GSU wala si AP. Kama wandani wake, tumeshangazwa na mabadiliko hayo na tunajiuliza nini hasa ilichangia hatua hiyo. Atwoli na Kibicho wanafaa waandikishe taarifa na DCI,” akasema Bi Kihika.

 

You can share this post!

Kuzikwa kwa BBI kwageuka pigo kwa Moi Bondeni

Ruto na Kalonzo kumenyana tena Ukambani