• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
WANTO WARUI: Mpango wa kulipa walimu wapya mapema ni wazo la busara

WANTO WARUI: Mpango wa kulipa walimu wapya mapema ni wazo la busara

NA WANTO WARUI

HATIMAYE Chama Cha Huduma kwa Walimu nchini (TSC) kimepanga kuanzisha utaratibu mpya wa kuwalipa walimu wapya wanaojiunga na TSC.

Haya yamesemwa na Katibu wa TSC, Bi Nancy Macharia. Kwa miaka mingi, walimu wamekuwa wakipitia dhiki na mateso mengi punde tu baada ya kuajiriwa kwani hawapokei mishahara yao mara moja.

Mishahara ya miezi ya mwanzo ya mwalimu mpya ambaye anaajiriwa na TSC imekuwa ikicheleweshwa kwa muda wa miezi mitatu hadi sita huku walimu hao ambao hawana pesa za kujisimamia wakipitia dhiki na mateso mengi katika kipindi hicho.

Wengi wao iliwabidi kukopa huku na kule ili waweze kukimu mahitaji ya kila siku na kujinunulia mavazi ambayo yawiana na kanuni za mvao wa walimu.Hatua hii imekuwa mwiba kwa walimu wengi na hata baada ya kupewa mishahara yao kwa pamoja, haiwasaidii kwani huwa na madeni chungu nzima.

Akielezea sababu zilizosababisha mishahara hiyo kuchelewa kwa muda huo mrefu, Bi Macharia alisema kuwa mipango ya matayarisho ya faili za walimu hao ilichukua muda mrefu kupitia utendakazi wa awali. Kwa sasa, kuwepo kwa teknolojia kutawezesha mambo kufanywa kidijitali na kwa haraka.

Bi Macharia alielezea kuwa walimu wapya sasa watakuwa wakiripoti kwa njia ya mtandao, jambo ambalo litawezesha TSC kupanga na kuwalipa mishahara yao wa mwezi wa kwanza bila kuchelewa.

Aidha, Katibu huyo wa TSC amesema kuwa masuala mengine kama ya uhamisho wa walimu na mabadiliko ya kazi yatakuwa yakifanywa kupitia mtandaoni ili kuepuka kuchukua muda mrefu sana kabla hayajatekelezwa.

Hivi ni kusema kuwa mwelekeo ambao TSC inachukua utaendelea kuboresha elimu ikizingatiwa kuwa walimu wengi wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu sana ikiwemo ukosefu wa mishahara kwa wakati ufaao, kulipwa mishahara duni, kuishi katika mazingira yasiyofaa, ukosefu wa usalama katika baadhi ya maeneo miongoni mwa mambo mengine.Utoaji wa elimu bora unategemea sana mwalimu na mazingira ya kazi.

Hali mbaya za utoaji wa elimu nchini zimekuwa zikichangia sana matokeo mabaya kwa wanafunzi huku walimu wengi wakiishi katika nyumba duni na hata kushindwa kuwajibikia familia zao ipasavyo.

Ikiwa TSC pamoja na Wizara ya Elimu zitashirikiana kufikiria zaidi kuhusu matatizo yanayowatinga walimu kote nchini, kisha idara hizi zitafute njia bora za kutatua matatizo hayo, basi bila shaka kiwango cha elimu nchini kitapanda.

Mpango huu ambao umechukuliwa na TSC wa kuwalipa walimu wapya punde tu baada ya mwezi wa kwanza unafaa kuwa tu mojawapo ya hatua za kuboresha huduma kwa walimu wote kote nchini.

You can share this post!

Korti yaruhusu kaunti izike miili iliyotelekezwa kwa zaidi...

LEONARD ONYANGO: Wakuu wa shule waliotafuna mabilioni...