• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
HASLA BANDIA

HASLA BANDIA

Na CHARLES WASONGA

HATUA ya Wabunge kuagiza Waziri wa Usalama, Fred Matiang’i na maafisa wakuu katika idara ya polisi kufika mbele yao jana imeanika Naibu Rais William Ruto kama bwanyenye mkubwa anayejisawiri kijanja kama mtu wa tabaka la chini maarufu kama hasla.?

Akitoa maelezo mbele ya wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Usalama kuhusu ulinzi anaopewa Dkt Ruto, Dkt Matiang’i aliorodhesha mali ya naibu huyo wa rais inayolindwa na jumla ya polisi 51.

Mali hiyo inajumuisha mashamba makubwa katika kaunti za Laikipia, Narok na Taita Taveta, hoteli mbili zilizoko Nairobi na Mombasa miongoni mwa mali nyinginezo zilizotapakaa sehemu mbalimbali nchini na kuwa chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa usalama kutoka vitengo mbalimbali.

Waziri Matiang’i jana aliwaambia wanachama wa kamati hiyo kwamba, jumla ya maafisa 257 wanatoa ulinzi kwa Naibu Rais na baadhi ya mali anazomiliki.

Dkt Matiang’i alipuuzilia madai kwamba usalama wa Dkt Ruto sio thabiti kutokana na kubadilishwa kwa walinzi katika makao yake rasmi mtaani Karen, Nairobi. Katika mabadiliko hayo, maafisa wa GSU waliondolewa na mahala pao kuchukuliwa na askari tawala (AP) kutoka kitengo cha kulinda majengo ya serikali (GBC).

“Wakati huu Naibu Rais anapata ulinzi kutoka maafisa 74 wa GSU wa kikosi maalum cha kulinda rais (PEU). Maafisa wengine 183 kutoka vikosi mbalimbali wanalinda makazi na mali yake,” akaambia kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Limuru, Peter Mwathi katika majengo ya bunge.?

“Mali hizo ni kama vile; kampuni ya gesi ya Kitengela yenye maafisa sita wa polisi, hoteli ya Weston Nairobi inalindwa na polisi sita, Shamba la Murumbi lililoko Transmara, kaunti ya Nairobi (lenye ukubwa wa hekta 395) lina polisi sita, Shamba la ADC Mutara Ranch (lenye ukubwa wa ekari 1500) limetengewa polisi sita na hoteli ya Dolphin, Mombasa inalindwa na polisi sita.”

“Shamba la Mata, liliko kaunti ya Taita Taveta lenye ukubwa wa ekari 2537 linalindwa na polisi sita, makazi ya kibinafisi katika mtaa wa Elgon View, Eldoret yanalindwa na polisi wanne, shamba la ufugaji kuku la Koitalel Poultry, Eldoret linalindwa na maafisa wanne wa polisi, makazi ya kibinafsi ya Kosachei mjini Eldoret yanalindwa na maafisa watatu wa magereza na kampuni ya Kwae Island Development Ltd, iliyoko Uwanja wa Wilson ambako kuna helikopta tano za Naibu Rais imetengewa polisi watano,” Dkt Matiang’i akawaambia wabunge hao.

Waziri huyo alisema orodha ya mali aliwasomea wabunge jana ni sehemu tu ya mali ya Dkt Ruto ambaye alimtaja kama afisa anayepewa ulinzi mkali zaidi kuliko Makamu wa Rais ambao wamehudumu tangu 1963 hadi 2013.

“Hizi ni sehemu tu ya mali ambayo Naibu Rais anamiliki na ambayo serikali inawajibu wa kulinda baada ya kupokea ombi kutoka kwa kiongozi huyo,” Dkt Matiang’i akawambia wabunge hao.

Dkt Matiang’i alikuwa ameandamana na Katibu katika Wizara hiyo Karanja Kibicho, Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai, Mkurugezi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti na maafisa wengine wakuu katika idara ya polisi na wizara yake.

Dkt Ruto amekuwa akijnadi kama mtu wa kawaida na masikini ambaye alipata mali yake kidogo kutokana na bidii yake katika biashara ndogo ndogo kama vile uuzaji kuku kule nyumbani kwao Turbo, kaunti ya Uasin Gishu.

Naibu Rais amekuwa akijihusisha na watu wa tabaka la chini na walala hoi kama vile mama mboga, wahudumu wa boda boda, wabeba mizigo kwa kutumia mikokoteni na wafanyabiashara wengine wadogo, anaowaita kama mahasla.

Katika kampeni yake ya kutaka achaguliwe kuwa Rais wa tano wa Kenya, Dkt Ruto amebuni mfumo wa ukuzaji uchumi kuanzia chini, maarufu kwa kimombo kama “bottom-up ecomonic model”.?

“Serikali ambayo tutaunda 2022, Mungu akipenda, itakuwa ni ya hawa mahasla wote. Itakuwa serikali ya Mama Mboga, waendeshaji mikokoteni, watu wa boda boda na wachuuzi. Itakuwa ni serikali ya kuwainua ili nao wahisi kuwa Kenya hii ni yao,” Dkt Ruto alisema Jumanne alipokutana na ujumbe kutoka eneo bunge la Dagoreti Kusini katika makazi yake rasmi ya Karen, Nairobi.

Naye Seneta wa Nandi Samson Cherargei alipuuzilia mbali madai ya Dkt Matiang’i akisema yalichochewa kisiasa.

“Hao maafisa wa usalama walikuwa wakicheza siasa tu. Ukweli ni kwamba usalama wa Naibu Rais umepunguzwa. Maelezo ambayo walitoa hayana msingi wowote,” akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge.

Katibu wa Mawasiliano katika Afisi ya Naibu Rais David Mugonyi alipuuzilia mbali orodha ya mali ambayo Dkt Matiang’i alidai inamilikiwa na Dkt Ruto.

“Ni aibu kwamba Waziri alitumia bunge kama jukwaa la kuendeleza uwongo na kuikosea heshima Afisi ya Naibu Rais kwa kuchapisha takwimu za uwongo. Ukweli ni kwamba nyingi za mali zilizoorodhesha hazimilikiwi na Naibu Rais,” akasema Bw Mugonyi, bila kutoa ufafanuzi zaidi.

 

You can share this post!

Kituo cha polisi kujengwa eneo la Gatong’ora

Polisi sita wakana kuua ndugu wawili Embu agosti 1, 2021