• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Kamishna ataka serikali impe ndege ya kusaka wanafunzi

Kamishna ataka serikali impe ndege ya kusaka wanafunzi

NA MWANDISHI WETU

KAMISHNA wa Kaunti ya Baringo Henry Wafula ameitaka serikali kumpa helikopta ili awasake watahiniwa wa KCPE mwaka jana ambao hawajajiunga na kidato cha kwanza katika vijiji vya kaunti hiyo.

Bw Wafula na Mkurugenzi wa Elimu wa kaunti hiyo Mwasaru Mwashegwa walisema kwamba wanahitaji helikopta kwa kuwa barabara zinazoelekea maeneo ya vijiji hazipitiki, jambo linalowatatiza kuwafikia watahiniwa wote.

Mnamo Alhamisi, maafisa hao walifanya msako katika Kaunti Ndogo za Eldama Ravine na Mogotio kuhakikisha watahiniwa wote wa KCPE, wamejiunga na shule za upili.

Haya yanajiri siku chache baada ya Waziri wa Elimu George Magoha kutembelea kaunti hiyo na kugundua kwamba asilimia kubwa ya wanafunzi waliofanya KCPE hawajajiunga na sekondari.Bw Magoha aliwapa muda wa wiki moja kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi amejiunga na kidato cha kwanza.

“Kaunti yetu ni kubwa sana. Vijiji vingine katika maeneo ya mbali kama Tiaty havipitiki kwa barabara. Hii inafanya iwe vigumu kutimiza amri ya serikali ya kuhakikisha watahiniwa wote wa KCPE wamejiunga na Kidato cha Kwanza,” akasema Bw Wafula.

“Kwa sababu ya usalama, tunaomba Bw Magoha atukabidhi helikopta ili tuweze kufikia maeneo kama Tiaty,” akaongeza Bw Wafula.

Kamishna huyo alisema asilimia 93 ya watahiniwa tayari wamejiunga na Kidato cha Kwanza katika Kaunti Ndogo ya Eldama Ravine.Alisema wanafanya juu chini ili kuhakikisha watahiniwa wote wamejiunga na Sekondari kufikia Ijumaa.

“Tunalenga kuwafikia watahiniwa wote ambao hawajajiunga na shule za upili. Tuna shida kufika eneo la Tiaty ila tunafanya juu chini ili tuwafikie,” akasema Bw Wafula.

Hata hivyo, aliwaonya wazazi kutoka Tiaty dhidi ya kutumia ukosefu wa usalama katika eneo hilo kusalia na watoto wao nyumbani.

Haya yanajiri baada ya Bw Magoha kutembelea kaunti mbalimbali ili kuhakikisha kuwa watahiniwa wote wanajiunga na shule za upili.Bw Mogoha alisema anatembelea kaunti hizo binafsi kwa kuwa hawaamini maafisa walio katika kaunti hizo.

You can share this post!

Mahakama yakataa ombi la maafisa sita wa polisi...

Raila anyenyekea wazito Mlima Kenya