• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 PM
Makahaba kutoka UG na TZ wamiminika Narok kuvuna hela za ngano

Makahaba kutoka UG na TZ wamiminika Narok kuvuna hela za ngano

Na GEORGE SAYAGIE

MAMIA ya makahaba wakiwemo wa kutoka nchi jirani wameingia Kaunti ya Narok kuvuna mapato kutoka kwa wakulima wa ngano ambao wameanza kulipwa.

Makahaba hao pia wanaotea watalii walioanza kwenda katika mbuga ya wanyamapori ya Maasai Mara kushuhudia uhamiaji wa kongoni.

Baadhi yao wametoka nchi jirani za Uganda na Tanzania huku wengine wakitoka maeneo ya Nakuru, Eldoret, Kericho, Nairobi, eneo la Kati na Mombasa.

Kwa kawaida wao hujaa Narok msimu huu ambapo wakulima wa ngano wanauza mazao yao kwa wingi.

Wafanyabiashara waliohojiwa na Taifa Leo walisema hali hii husaidia pia biashara zingine kufaidika ingawa walitaka wakulima wajihadhari.

“Kila mwaka msimu huu huwa ni wa faida kwa sababu ya utalii katika Maasai Mara na uvunaji wa ngano katika kaunti, lakini watu wengi wanaokuja huwa wana nia mbaya,” akasema Bw Joseph Kamau, mfanyabiashara wa ngano.

“Kuna makahaba ambao huja katika msimu wa kuvuna pekee. Wao huenda Kericho wakati wakulima wa chai wanapolipwa bonasi Novemba kisha hujazana hapa Julai na Agosti. Ikifika Septemba wataenda kwingine,” akaeleza.

Mkuu wa polisi wa Narok, Bw Joseph Kisombe, alisema polisi wameimarisha upigaji doria katika maeneo mbalimbali msimu huu ikiwemo Narok mjini, Suswa, Ntulele, Melili na Ololulung’a ili kuzuia ongezeko la uhalifu msimu huu.

Bw Kisombe alisema wamewahi kupokea malalamishi kadhaa kutoka kwa wakulima wa ngano na wateja wengine ambao waliibiwa pesa na mali nyingine baada ya kutiliwa dawa za kulevya na makahaba hao.

“Polisi watakuwa macho kuzuia uhalifu wowote ikiwemo jinsi wakulima wa ngano wanvyotiliwa dawa za kulevya,” akasema.

Visa vya watu kutiliwa dawa za kulevya katika msimu huu huongezeka katika eneo hilo ingawa vingi huwa haviripotiwi, pengine kutokana na jinsi wanaume husika wanavyotaka wasijulikane walihadaiwa na makahaba.

You can share this post!

Kuria ajuta kumsimanga Raila

Kuna mabilioni ya miradi mipya, Ruto asema

adminleo