• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Ruto kukabiliwa na mtihani mkali 2022 akiepuka miungano

Ruto kukabiliwa na mtihani mkali 2022 akiepuka miungano

Na WANDERI KAMAU

HATUA ya Naibu Rais William Ruto kusema kwamba hatajiunga na muungano ya kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022, imeibua maswali kuhusu ikiwa ataibuka mshindi kwenye uchaguzi huo bila muungano wa kisiasa.

Chama cha UDA, ambacho kinahusishwa na Dkt Ruto, kilisema kwamba hakitaandikisha mkataba wowote wa kisiasa na chama kingine kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Badala yake, chama hicho kilisema kuwa kitakaribisha muungano wa kisiasa tu na vyama mbalimbali baada ya uchaguzi, ili kubaini nguvu zake za kisiasa.

Kauli hiyo inajiri huku viongozi kadhaa walioonekana kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto wakianza kujitenga naye.

Katika mahojiano, mbunge Rigathi Gachagua (Mathira) alisema kuwa viongozi wanaosisitiza kuunganisha vyama vyao na UDA wanapaswa kufanya hivyo baada ya uchaguzi ujao “ili nguvu zao za kisiasa ziweze kudhihirika ifaavyo.”

“Hatukatai kuungana na vyama vingine vya kisiasa. Hata hivyo, lazima tufahamu nguvu na ushawishi vilivyo navyo. Baadhi ya vyama vinavyosisitiza kuunda muungano wa kisiasa na UDA havishikilii hata kiti kimoja cha uwakilishi. Katika hali hiyo, itakuwa vigumu kuunda muungano,” akasema Bw Gachagua.

Mbunge huyo alisema ni vigumu kwa makubaliano ya kisiasa kufanyika katika mazingira hayo, kwani miafaka ya kisiasa huzingatia ushawishi wa chama husika.

Baadhi ya viongozi wanaoegemea mrengo wa Dkt Ruto ambao wamesisitiza kwamba hawatavunja vyama vyao ni aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri na mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria.

Bw Kiunjuri anaongoza chama cha The Service Party (TSP) huku Bw Kuria akiongoza Chama cha Kazi (CCK).Katika mahojiano, Katibu Mkuu wa TSP, Bw Karungo Thang’wa, alisema kuwa sawa na vyama vingine, lengo lao ni kuwa “chama cha kitaifa.”

Bw Thang’wa alisema kuwa ingawa miungano ya kisiasa ni muhimu katika siasa za Kenya kwa sasa, “hawatakataa kushirikiana na watu na vyama walio na maono sawa.”

“Sisi ni chama chenye mizizi katika kila sehemu nchini. Licha ya kuendelea kuwafikia wananchi katika kila sehemu ya nchi, hatujafunga mlango kushirikiana na viongozi wengine wenye maono sawa nasi,” akasema.

Msimamo wa UDA umezua hisia mseto miongoni mwa vyama vinavyoonekana kuwa washirika, baadhi vikionekana kuwa katika njiapanda.

Baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakidai kwamba msimamo huo ni mpango wa watu walio karibu na Dkt Ruto kuwafungia nje watu wanaozua ushindani wa kisiasa dhidi yao.

Kulingana na wadadisi wa siasa, kuna uwezekano mwelekeo huo ndio umewafanya baadhi ya washirika wa Dkt Ruto kuanza kushinikiza uwepo wa chama kimoja cha kikanda katika eneo la Mlima Kenya.

You can share this post!

Sijajiunga na DP – Muturi

Falcao arejea Uhispania kuchezea Rayo Vallecano baada ya...