• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 7:50 AM
Kiunjuri ashauri Ruto ashirikiane na vyama vingine

Kiunjuri ashauri Ruto ashirikiane na vyama vingine

Na JAMES MURIMI

KIONGOZI wa chama cha TSP, Mwangi Kiunjuri, amemrai Naibu Rais William Ruto kubuni ushirikiano wa kisiasa na viongozi wa vyama vingine ikiwa anataka kupata uungwaji mkono eneo la Mlima Kenya mwaka 2022.

Akihutubu Jumapili wakati wa hafla ya ibada katika Kanisa la ACK St Andrews mjini Nanyuki, Bw Kiunjuri alionya kwamba ni mapema sana kwa kiongozi yeyote kudai kwamba amejizolea uungwaji mkono wa eneo hilo.

Badala yake, alisema kuwa mbinu nzuri ya kupenya kisiasa katika ukanda huo ni kuwaunganisha viongozi na vyama vya kisiasa.

“Ni mapema sana kusema ushaukwea Mlima. Mlima huu ni mrefu sana na una barafu kileleni mwake. Hali ya anga huenda ikawa si ya kuridhisha. Kwa hivyo, ni vizuri kuendelea kubuni ushirikiano na watu. Usifikiri kuwa umefaulu,” akasema Bw Kiunjuri, kwenye ujumbe aliotoa kimafumbo.

Bw Kiunjuri, aliyehudumu kama Waziri wa Kilimo, alisema kuwa hatavunja chama chake, ijapokuwa yuko tayari kujiunga na miungano ya kisiasa pakiwa na uwezekano.

“Mimi si mpumbavu kubuni TSP. Hili litatusaidia kuitisha haki yetu kirasilimali wakati wa kubuniwa kwa serikali ijayo,” akasema.

Bw Kiunjuri alitoa kauli hiyo kufuatia matamshi ya washirika wa Dkt Ruto katika eneo hilo kuwa watashinikiza kushirikishwa serikalini kupitia chama cha UDA pekee.

Jumamosi, wabunge hao walisema chama hicho hakitajiunga na muungano wowote wa kisiasa kwenye azma yake kuwania urais 2022.

Wabunge 50 kutoka eneo hilo wikendi walipitisha kauli ya pamoja kumuunga mkono kuwania urais kupitia tiketi ya UDA.

Wabunge walisema kuwa watashirikiana na miungano mingine tu ikiwa itajiunga nao ili kuhakikisha Dkt Ruto amepata ushindi.

You can share this post!

Baba ndani kwa madai ya kumchoma mwanawe

GUMZO LA SPOTI: Ole Gunnar alizuia mastaa 5 kuaga klabu