• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 8:55 AM
Chama cha Kingi chaanza kuvutia wanachama

Chama cha Kingi chaanza kuvutia wanachama

Na MAUREEN ONGALA

MAMIA ya wakazi wa Kilifi walijitokeza kujisajili kuwa wanachama wa Chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kilichoanzishwa hivi majuzi Pwani.

Usajili huo ulizinduliwa wikendi katika afisi ya chama hicho iliyo eneo la Bofa, Kaunti ya Kilifi ukavutia idadi kubwa ya wananchi.

Chama hicho ambacho kinahusishwa na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, kimeungwa mkono na baadhi ya madiwani ambao wangali ni wanachama wa ODM.

Kando na madiwani, Mbunge wa Magarini, Bw Michael Kingi, ndiye mbunge pekee ambaye ametangaza wazi kukiunga mkono kufikia sasa.

Uundaji wa PAA umetoa changamoto kwa Chama cha ODM ambacho kimedhibiti siasa za eneo la Pwani pakubwa kwa miaka mingi kupanga mikakati yake upya.

Vile vile, Naibu Rais ambaye amefanya kampeni nyingi Kilifi kupigia debe Chama cha United Democratic Alliance (UDA), huenda akalazimika kujipanga upya.

Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya, ambaye huegemea upande wa Dkt Ruto, alisisitiza kuwa chama hicho hakina maono yoyote mapya kwa Wapwani na kitaifa.

Mbunge huyo aliyechaguliwa kupitia kwa ODM alikashifu uundaji wa chama hicho akidai kuwa kinalenga kutumia vibaya hisia za Wapwani kwa manufaa ya viongozi ambao hawataki kutokomea baada ya 2022.

Kulingana naye, wanasiasa wanafaa wawe wanatilia maanani hitaji la kuunganisha Wapwani na jamii nyingine zote kitaifa badala ya kuunda vyama ambavyo vinaonekana kuwa vya kieneo.

“Marehemu Ronald Ngala hakuungana na Wagiriama kuunda KADU, bali alishirikiana na Daniel Moi, Jaramogi Oginga na Masinde Muliro. Waliungana pamoja na Wakenya wengine,” akasema.

Wanasiasa ambao hutetea uundaji wa chama kikubwa kilicho na mizizi yake Pwani wakiongozwa na Gavana Kingi, husisitiza kuwa hilo ni muhimu ili eneo hilo lipate usemi sawa na maeneo mengine ya nchi wakati viongozi wa kitaifa wanapojadiliana kuhusu masuala ya utawala na maendeleo ya nchi.

Kufikia sasa, Pwani bado imebaki nyuma wakati ambapo vigogo wa kisiasa wa maeneo mengine wanaendeleza mashauriano ya kuunda miungano.

Wiki chache zilizopita, Gavana Kingi alikataa wito wa Dkt Ruto na wandani wake waliomtaka ajiunge na UDA, akisisitiza ni lazima kuwe na umoja baina ya viongozi na wakazi wa Pwani kisiasa kabla waingie katika miungano ya kitaifa.

Wakili George Kithi, anayepanga kuwania Useneta Kilifi, alisifu uundaji wa chama cha Pwani ila akaonya kuwa, bado kuna hatari kwa chama hicho kulegea jinsi vyama vingine vya Pwani vilivyoishia kutopata umaarufu kitaifa.

“Kitu chochote kinachoanzishwa nyumbani ni kizuri, lakini onyo ambalo ningependa kutoa ni kwamba, matatizo yaliyokumba vyama vilivyotangulia bado yapo. Demokrasia ni lazima ikumbatiwe, ilhali tayari tunashuhudia hali ambapo PAA inahusishwa na watu wachache,” akasema.

Baadhi ya wakazi waliojisajili kuwa wanachama wa PAA walieleza matumaini yao kwamba chama hicho kitawakilisha vyema masilahi ya eneo la Pwani kitaifa.

Hata hivyo, walionya viongozi dhidi ya kukitumia kwa manufaa yao wenyewe.

You can share this post!

Watu 10,000 pekee kuhudhuria sherehe za Mashujaa Kirinyaga

WASONGA: Raia wasibebeshwe mzigo wa kulinda mali ya wakuu