• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 8:55 AM
WASONGA: Raia wasibebeshwe mzigo wa kulinda mali ya wakuu

WASONGA: Raia wasibebeshwe mzigo wa kulinda mali ya wakuu

Na CHARLES WASONGA

UFICHUZI wa juzi kwamba hata mali ya kibinafsi ya Naibu Rais William Ruto inalindwa na maafisa wa usalama wa serikali una maana kuwa kuna pengo la kisheria katika sekta ya ulinzi wa watu mashuhuri nchini.

Kwamba afisa yeyote wa serikali anaweza kuwasilisha ombi kwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) akitaka walinzi zaidi na akapewa inaonyesha namna ambavyo maafisa fulani huwatumia vibaya maafisa wa usalama.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti ambayo Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i aliwasilisha bungeni Alhamisi wiki jana ambapo alidai kuwa Naibu Rais William Ruto pekee hupewa ulinzi na maafisa 257.

Dkt Matiang’i aliwaambia wabunge wanachama wa Kamati kuhusu Usalama na Utawala kwamba 51 kati ya maafisa hao wanalinda mali ya Dkt Ruto zilizoko maeneo mbalimbali nchini.

Waziri alifichua kuwa kwa ujumla, takriban maafisa 4,000 wa usalama wanatumiwa kutoa ulinzi kwa watu mashuhuri nchini; kuanzia Rais hadi maafisa wengine wakuu katika nguzo tatu za serikali; Bunge, Idara ya Mahakama na Afisi Kuu.

Kwa mtazamo wangu, ni sawa kwa Watu Mashahuri Nchini (VIPs) kupewa ulinzi kwa misingi ya majukumu mazito ya kitaifa wanayotekeleza.

Hata hivyo, sidhani kwamba mlipa ushuru anapaswa kubebeshwa gharama ya ulinzi wa mali yao ya kibinafsi.

Ninachomaanisha ni kwamba maafisa wa usalama kutoka vitengo mbalimbali hawafai kulinda mali kama hii!

Mali ambayo maafisa wa polisi wanafaa kulinda ni ile ya umma lakini ambayo inatumiwa na VIPs hawa wanapotekeleza majukumu ya afisi zao kwa manufaa ya umma.

Maafisa hao wanafaa wagharamie ulinzi wa mali yao ya kibinafsi kwa kukodi huduma hizo kutoka kwa kampuni za kibinafsi za ulinzi.

Kadhalika, walipie huduma hizo ikiwa ni sharti mali yao ilindwe na maafisa wa polisi.Kwa hivyo, naunga mkono pendekezo la wabunge wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati kuhusu Usalama Peter Mwathi, kwamba Wizara ya Usalama ibuni sheria itakayolainisha suala zima la ulinzi wa watu mashuhuri katika sekta ya umma.

Idadi ya maafisa wa usalama wanaowalinda VIPs wote inafaa kudhibitiwa, si tu Dkt Ruto. Hii itatoa nafasi kwa maafisa wengine kutoa huduma kwa Wakenya ambao usalama wao uko hatarini katika sehemu mbalimbali nchini.

Jumla

Ikiwa Dkt Ruto pekee analindwa na jumla ya maafisa 257, ninaamini kuwa wale wanaolinda Rais Uhuru Kenyatta na mali yake ni karibu mara tatu ya idadi hii.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Dkt Matiang’i bungeni wiki jana, idadi ya maafisa wa polisi nchini ni 102,233.

Hii ina maana kuwa, kwa wastani nchini Kenya polisi mmoja analinda raia 600.Hii ni idadi ya juu zaidi kuliko kiwango kilichowekwa na Umoja wa Mataifa (UN) cha afisa mmoja kwa raia 450 (1:450).

Kwa misingi ya takwimu hizi, ni wazi kuwa Kenya inakabiliwa na uhaba wa maafisa wa kutoa usalama wa ndani.

Kwa hivyo, maafisa wachache walioko wanafaa kutumiwa vizuri na kwa manufaa ya Wakenya wote; walio mamlakani na raia wa kawaida.

Kwa hivyo, ipo haja kwa idadi ya maafisa wa usalama wanaowalinda VIPs kama vile Rais, Naibu Rais, Mawaziri, Majaji wa Mahakama, Maspika wa Mabunge Mawili ya Kitaifa, Magavana na maafisa wengine wanaoshikilia vyeo vya juu katika ngazi zote za serikali ipunguzwe.

Kwa mujibu wa kipengele cha 43 cha Katiba ya sasa, ni wajibu wa Serikali Kuu kutoa usalama kwa Wakenya wote, bila kujali vyeo au hadhi yao katika jamii.

You can share this post!

Chama cha Kingi chaanza kuvutia wanachama

WARUI: Serikali iharakishe utoaji chanjo kuokoa sekta ya...